Kagere waifuata Stars kufuzu 2022

12Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kagere waifuata Stars kufuzu 2022

MSHAMBULIAJI wa Klabu ya Simba, Meddie Kagere, ameiongoza timu yake ya Taifa ya Rwanda kuungana na Taifa Stars kuwa miongoni mwa timu zilizofuzu hatua ya makundi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 baada ya kuifungia mabao mawili wakati ikiichapa Shelisheli 7-0 juzi.

MSHAMBULIAJI wa Klabu ya Simba, Meddie Kagere.

Matokeo hayo yanaifanya Rwanda kuitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 10-0 baada ya Alhamisi iliyopita kwenye mechi ya awali kushinda 3-0 ugenini huku Kagere akitupia moja katika ushindi huo.

Katika mchezo wa juzi uliopigwa Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, mbali na Kagere aliyeziona nyavu dakika ya 27 na 51, mabao mengine yalifungwa na Jacques Tuyisenge dakika ya 28 na 34, Yanick Mukunzi dakika ya 57 na Muhadjir Hakizimana dakika ya 79.

Hakizimana na Mukunzi pia walikuwa miongoni mwa wafungaji waliocheka na nyavu katika mechi ya awali ugenini, hivyo sasa Rwanda inayonolewa na kocha mzawa Vincent Mashami inaungana na Taifa Stars iliyoitoa Burundi kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2, kusubiri kujua makundi watakayoangukia kuwania kufuzu fainali hizo.

Kagere ambaye juzi alitangazwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti na Bodi ya Ligi Kuu Bara, ameuanza msimu huu kwa mafanikio makubwa kwani katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara pia alitupia mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho wakati wakishinda 3-1 dhidi ya JKT Tanzania.