Wanawake 4, mwanamume jela kwa ukahaba

12Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Wanawake 4, mwanamume jela kwa ukahaba

WANAWAKE wanne na mwanamume mmoja  anayedaiwa kuwa mteja wao wamehukumiwa kifungo cha miezi sita jela na Mahakama ya Mwanzo ya Makole, jijini hapa, ikiwamo kuchapwa viboko vitatu wakati wa kuingia.

Kamanda wa Polisi, Gilles Muroto.

Hukumu hiyo inafuatia Jeshi la polisi mkoani hapa kuendelea na msako wa kuwakamata wanawake wanaodaiwa kuwa makahaba katika maeneo mbalimbali wanayofanya kazi ya kuuza miili yao kama sehemu ya kujiingizia kipato.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Kamanda wa Polisi, Gilles Muroto, alisema msako wa kinadada wanaojiuza miili yao unaendelea na kuwataka wanaofanya biashara hiyo kuacha mara moja.

Kamanda Muroto aliwataja waliokamatwa na kuhukumiwa kifungo hicho bila  faini na mmoja aliyehukumiwa miezi mitatu baada ya kukiri kosa, kuwa ni Erica George (24), Lucy Saibati (28), Joyce Ndekwa (30),

Hawa Said (28), na Grolia Michael (29).

Kamanda Muroto alisema, Septemba 8, mwaka huu katika Mtaa wa Uhindini, Kata ya Viwandani, watu hao walikamatwa kwa kosa la kufanya ukahaba kinyume na kifungu cha sheria namba 176 (a), f na g cha kanuni ya adhabu ya sura ya 16.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Mtaa wa Tofiki Uhindini, Alnoor Kassam, alisema baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, alikwenda kutoa taarifa polisi.

Alisema baadhi ya nyumba za kulala wageni ambazo zilikuwa zitumika kufanya biashara ya ngono,  wamiliki walizifunga kwa hiyari yao wenyewe.

Wakati huohuo, katika tukio lingine Kituo cha Polisi Kati, kilivamiwa na kundi la waendesha pikipiki (boda boda) zaidi ya 70 na kufanya fujo wakitaka kumtoa mahabusu, Bazil Mjungu, ili wampige baada ya kusababisha ajali ya gari na kumgonga bodaboda.

Waendesha bodaboda hao walitawanywa kwa Amani, lakini walikaidi amri ikiwamo kufunga barabara na kuzingira kituo cha polisi jambo lililosababisha askari kuwatawanya kwa kufyatua risasi hewani.

Watu 20 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na kufunguliwa mashtaka.

Alisema baada ya upelelezi kukamilika walifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka na kupatikana na hatia, walihuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kila mmoja bila faini.

Habari Kubwa