Hakimu mahakamani kwa tuhuma za rushwa

12Sep 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hakimu mahakamani kwa tuhuma za rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemfikisha mahakamani Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni, Omary Abdalah (40), kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 703,000.

Mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Theresia Mnjagira.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kuomba fedha hizo ili kumsaidia mlalamikaji kwenye kesi ya mirathi iliyofunguliwa mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Theresia Mnjagira, hakimu huyo amefikishwa mahakamani hapo pamoja na mfanyabiashara George Barongo (37), mkazi wa Kibamba kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa ya Sh. 498,000.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.

“Ilidaiwa kuwa mnamo Februari 12, 2017, Abdalah alimtaka mtoa taarifa ampe kiasi cha Sh. milioni moja ili aweze kumsadia kwenye kesi ya mirathi iliyokuwa mbele yake kinyume na utaratibu,” alisema.

Vile vile, alisema mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru Wilaya ya Kinondoni, Machi mosi, 2017, uchunguzi ulifanyika na kubaini kuwa tuhuma hizo ni za kweli na shauri hilo kuanza upya.

“Uchunguzi dhidi ya tuhuma zote mbili umekamilika na watuhumiwa wamefikishwa katika Mahakama ya Kinondoni kujibu tuhuma zinazowakabili,” alibainisha.

Katika hatua nyingine, Takukuru imemfikisha mahakamani Katibu wa Kamati ya Upimaji wa viwanja katika Mtaa wa Nyakasangwe, Nerbert Malevu (33) kwa kuomba rushwa ya Sh. milioni 2.5 na kupokea Sh. 500,000.

Ilidaiwa kuwa mnamo Agosti 14, mwaka huu, mtuhumiwa huyo alimtaka mtoa taarifa ampatie fedha hizo ili aweze kumpatia sehemu ya kiwanja ambacho kilikuwa cha mtoa taarifa kabla ya upimaji na kwa madai kuwa sehemu ya kiwanja hicho kiligaiwa mtu mwingine baada ya upimaji.

“Mlalamikaji alitoa taarifa Takukuru na Agosti 16, mwaka huu uchunguzi ulifanyika, tuliandaa mtego wa rushwa na kumkamata mtuhumiwa Agosti 20, majira ya saa 10 eneo la Mwenge Lukani Pub, baada ya kupokea Sh. 500,000,” alisema Mnjagira.

Alisema, Takukuru mkoani humo imetoa wito kwa watumishi wa umma na sekta binafsi wanaodhani hawawezi kutoa huduma bila ya kuomba na kupokea rushwa, kwamba waache tabia hiyo kwa kuwa ni kosa la jinai.

“Kwa wanaoendelea kukaidi Takukuru itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria bila huruma wala kumwonea haya mtu yeyote, tunawasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapodaiwa rushwa kwa lengo la kupata huduma kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi kupata huduma bila kutoa rushwa,” alisisitiza.

Kadhalika, aliwataka wananchi kuhudhuria kwa wingi vikao vya maandalizi ya urasimishaji wa viwanja ili kupata elimu ya taratibu za urasimishaji kwa lengo la kuondoa mwanya wa watendaji wachache wasio waadilifu kutumia udhaifu wa kutojua taratibu kuomba na kupokea rushwa,” alibainisha.

Habari Kubwa