Vitambulisho 8 kutumika uchaguzi wa serikali mitaa

12Sep 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vitambulisho 8 kutumika uchaguzi wa serikali mitaa

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetoa mwongozo wa uchaguzi wa viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa unataja vitambulisho vitakavyotumika kupigia kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Umetaja vitambulisho hivyo kuwa ni cha mpigakura, cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya bima ya afya, cha shule au chuo, mifuko ya hifadhi ya jamii, leseni ya udereva na cha taifa.

Pia mwongozo huo umeelezea sifa za mgombea, mpiga kura, siku ya kuanza kampeni pamoja na utaratibu wa kupiga kura.

Mwongozo vile vile umeelezea namna ya uandikishwaji wa wapigakura, uteuzi wa wasimamizi wa vituo, namna ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea utakavyofanyika.

Mwongozo huo uliowekwa kwenye tovuti ya wizara hiyo na kusainiwa na waziri mwenye dhamana, Selemani Jafo, pia ulieleza utaratibu wa kuwasilisha taarifa na matokeo ya uchaguzi huo.

Sifa za mpigakura

Umeeleza kuwa mpigakura katika uchaguzi huo ni lazima awe raia wa Tanzania, umri wa miaka 18 au zaidi, mkazi wa kijiji au kitongoji au mtaa ambao uchaguzi unafanyika, hana ugonjwa wa akili uliothibitishwa na daktari anayetambulika na serikali au Bodi ya Utabibu, amejiandikisha kupiga kura katika kitongoji au mtaa au kijiji husika.

Sifa za mgombea

Mwongozo pia ulitaja sifa za mgombea ni pamoja na; "raia wa Tanzania, ana umri wa miaka 21 au zaidi, anaweza kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza, ana shughuli halali ya kumwezesha kuishi, ni mwanachama wa chama cha siasa na amedhaminiwa na chama hicho, hajawahi kupatikana na hatia kwa kosa la utovu wa uaminifu katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi, hana ugonjwa wa akili.

Pia ilieleza kuwa fomu za kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi huo zitatolewa kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2019 kuanzia saa 1: 30 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.

Kampeni za uchaguzi

Ulieleza kuwa kampeni zitaanza Novemba 17 hadi 23, vyama vya siasa vyenye wagombea vinaweza kuwateua wanachama wake kuendesha kampeni kwa niaba ya wagombea wa vyama vyao.

Ulieleza kuwa kampeni za uchaguzi zitaanza saa mbili asubuhi na zitamalizika saa 12 jioni ya kila siku ya kampeni.

"Vyombo vya ulinzi na usalama hususani Jeshi la Polisi, Mgambo wenye sare au ofisa yeyote anayesimamia ulinzi, vitatumika katika kuhakikisha kunakuwapo na usalama na utulivu katika mikutano ya kampeni na wakati wa uchaguzi. Vikundi vya ulinzi vya jadi au binafsi au vya mashabiki wa vyama vya siasa havitaruhusiwa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au ya uchaguzi," ulieleza mwongozo huo.

Utaratibu wa kupiga kura

Mwongozo huo pia ulieleza kuwa kabla ya msimamizi wa kituo hajampatia mpiga kura karatasi za kupigia kura, atajiridhisha kama jina lake limeorodheshwa katika orodha ya wapigakura na baada ya kuridhika atamtaka mpigakura ajitambulishe kwa kutumia kitambulisho.

"Vitambulisho vitakavyotumika ni cha mpigakura, cha kazi, hati ya kusafiria, kadi ya bima ya afya, cha shule au chuo, cha mifuko ya hifadhi ya jamii, leseni ya udereva na cha taifa," ulieleza mwongozo huo.

Sifa za wasimamizi wasaidizi

Mwongozo huo ulieleza kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na maofisa wengine watakaoteuliwa watakuwa na sifa zifuatazo: "Wasiwe na dhamana au uongozi katika chama chochote cha siasa, wawe ni watumishi katika utumishi wa umma, wawe na uadilifu."

Ulieleza kuwa uteuzi wa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi utafanyika kuanzia Septemba 16 hadi 22, 2019.

Pingamizi la wagombea

Mwongozo huo ulieleza kuwa msimamizi wa uchaguzi atafanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za uongozi katika ngazi zote kuanzia Novemba 5, 2019.

"Mgombea au mtu aliyeomba kuteuliwa anaweza kuweka pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea na litawasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi kuanzia Novemba 5 hadi 6 , 2019 na msimamizi atasikiliza na kutoa uamuzi kuanzia Novemba 5 hadi 7.

Utaratibu wa kutangaza matokeo

Ulieleza kuwa matokeo uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa, yatatangazwa katika ngazi ya mtaa husika, na kwamba matokeo yatajazwa kwenye fomu maalum ambayo itasainiwa na wagombea au wawakilishi wao pamoja na msimamizi wa kituo na kubandikwa kwenye sehemu ya matangazo ya uchaguzi.

Ulieleza kuwa nakala za matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji na Wajumbe wa Halmashauri ya Vijiji kutoka katika vitongoji zitawasilishwa Ofisi ya Serikali ya Kijiji kwa ajili ya kujumlishwa na kutangazwa washindi.

Maoni ya vyama

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa Chama cha ACT- Wazalendo, Ado Shaibu, alisema walishirikishwa kwenye maoni katika mkutano uliofanyika Aprili, mjini Dodoma na uchambuzi ulifanyika kuhusu kanuni na waliunga mkono vitambulisho hivyo kutumika katika uchaguzi huo.

"Tulipendekeza kuwapo na wigo kwa wapigakura, hivyo hatuna wasiwasi na vitambulisho hivyo kutumika," alisema Shaibu.

Alisema kwenye kikao hicho walitoa maoni yao kwenye maeneo yenye shida na yasiyokuwa na shida.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tumaini Makene, alisema kikubwa vitambulisho hivyo vilenge kumsaidia mwananchi mwenye haki ya kupiga kura.

Alisema Chadema inachohitaji ni kuona mwananchi mwenye sifa anaruhusiwa kupiga kura kwa mujibu wa kanuni.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alisema: "Tunafuata sheria, kanuni na taratibu zinazotumika katika uchaguzi wa serikali za mitaa."

Habari Kubwa