NGO zakumbushwa kuweka ripoti za fedha wazi

12Sep 2019
Joseph Mwendapole
DAR ES SALAAM
Nipashe
NGO zakumbushwa kuweka ripoti za fedha wazi

SERIKALI imerudia kuzikumbusha asasi zisizo za kiserikali kuweka wazi mapato na matumizi yao pamoja na shughuli zote wanazofanya na imezionya zile zinazoendesha mambo yake kwa kificho.

Mratibu wa Kisekta kutoka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Andrew Komba.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Kisekta kutoka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Andrew Komba, wakati wa uzinduzi wa wiki ya asasi za kiraia iliyoandaliwa na Foundation for Civil Society (FCS).

Alisema nia ya serikali ni kutaka kujua kama shughuli za asasi hizo zinaenda sambamba na mipango yake ili kuondoa ukinzani unaoweza kutokea kwenye utekelezaji wa baadhi ya mambo baina ya pande hizo mbili.

“Tukisema asasi za kiraia ziweke wazi mambo yake haimaanishi upande wa fedha tu bali hata shughuli nzima mnazofanya kwasababu serikali inaweza ikawa inafanya hivi huku nyinyi mnafanya kinyume chake,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga, alisema zaidi ya asasi za kiraia 15 chini ya uratibu wa FCS zinaandaa wiki ya asasi za kiraia itakayofanyika mwezi Oktoba, mkoani Dodoma.

Kiwanga alisema wiki ya azaki inalenga kuunda na kuimarisha muundo endelevu wa kuleta ukuaji unaochagizwa na uhusishwaji makini wa asasi za kiraia katika azma ya kuiletea Tanzania maendeleo.

Kiwanga alisema katika wiki ya asasi za kiraia kutakuwa na matukio mbalimbali yenye lengo la kupaza sauti masuala mbalimbali na kuwezesha utambuzi wa maeneo ya ushirikiano.

Alisema kutakuwa na ufunguzi wa maonyesho ya kazi za asasi mbalimbali yanayolenga kuwahusisha zaidi wananchi wa kawaida, warsha za pamoja na zile za wenye mahitaji maalum na utoaji wa tuzo.

Alisema mwaka jana tukio kama hilo lilifanyika mkoani Dodoma na kaulimbiu yake ilikuwa juhudi za ujenzi wa viwanda Tanzania, watu, sera na utekelezaji na lilileta pamoja washiriki zaidi ya 600 kutoka asasi 400.

Habari Kubwa