Kelvin amfuata Samatta Ubelgiji

14Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kelvin amfuata Samatta Ubelgiji

NYOTA ya wachezaji wa Tanzania kucheza soka la kulipwa Ulaya inaendelea kung'ara baada mshambuliaji chipukizi, Kelvin John, kupata mwaliko wa kwenda katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, ambayo anaichezea nahodha wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), Mbwana Samatta, imefahamika.

Mshambuliaji chipukizi, Kelvin John.

Kwa muda mrefu Kelvin licha ya kujumuishwa mara kwa mara kwenye timu za taifa, hakuwa na timu ya kuichezea hali iliyopelekea wadau wengi wa soka kupiga kelele wakitaka mchezaji huyo apate klabu ili kutunza kipaji chake huku  mipango ya kusaka klabu Ulaya ikiendelea.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zinaeleza kuwa KRC Genk imetuma barua kwa ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania ikielezea kumuita kinda huyo kwenda nchini humu kwa ajili ya majadiliano ya kusaini mkataba.

Nipashe imeiona nakala ya barua hiyo ambayo pia ilikuwa inampatia viza ya kuingia nchini humo kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa kuanza kucheza soka la kulipwa.

Barua hiyo pia imeelezea mahali ambapo mshambuliaji huyo atafikia na klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji ikiweka wazi, ndiyo italipa gharama zote za usafiri na malazi kwa muda wote atakaokuwa nchini humo.

Mshambuliaji huyo alianza kung'ara akiwa na kikosi cha Timu ya Taifa ya Vijana ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), ambacho kilishiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON U-17 2019), ambazo zilifanyika Aprili mwaka huu hapa jijini.

Habari Kubwa