Majaliwa asimamisha watumishi kisa bil. 1.3/-

16Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Majaliwa asimamisha watumishi kisa bil. 1.3/-

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewasimamisha kazi watumishi saba katika halmashauri mbili za Wilaya ya Kilombero kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha zaidi ya Sh. bilioni 1.3 za makusanyo ya mapato ya ndani.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza warejeshe fedha hizo ndani ya siku tatu kabla hajamaliza ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Watumishi hao ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Fransis Ndulane, anayedaiwa Sh. milioni tano alizoingiziwa katika akaunti yake bila maelezo yoyote.

Waziri Mkuu aliwasimamisha kazi watumishi hao jana wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa katika siku ya pili za ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Amesema: “Mkoa mzima wa Morogoro umekuwa na tatizo la upotevu wa mapato, fedha zinakusanywa zinapita mikononi mwa watu hazifiki benki, hii ni shida, hatutavumilia.”

Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kipindi cha mwaka 2016 hadi Juni 2019, katika mji wa Ifakara, makusanyo yalikuwa ni Sh. bilioni 2.7, ambapo fedha iliopelekwa benki ni Sh. bilioni 1.9, na kwamba kiasi cha Sh. milioni 727 hazijulikani zilikoenda.

Alisema katika mitambo kumi ya ukusanyaji wa mapato iliokaguliwa, imeonyesha kiasi cha Sh. milioni 348 zilizokusanywa hazikupelekwa benki, hivyo kuishia mikononi mwa watu.

Waziri Mkuu alisema katika uchunguzi huo, ilibainika fedha hizo ziliingizwa katika akaunti mbalimbali za watumishi wa halmashauri hizo kutoka kwa mtendaji wa Kata ya Viwanja 60 katika Mji wa Ifakara, Gregory Midas.

Watumishi hao ni Reina Mrema, ambaye anadaiwa kuchukua Sh. milioni  298, Haile Njitango milioni 73, Linus Mdembo kiasi cha Sh. milioni mbili kwa kushirikiana na mtendaji huyo wa kata.

Waziri Mkuu aliagiza Mkuu wa Kitengo cha Tehama katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, John Mvanga, ambaye ndiye alibaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha hizo na baadaye kusimamishwa kazi, arejeshwe kazini mara moja na asibughudhiwe.

“Mlimsimamisha kazi kwa sababu mlijua amegundua madudu yenu, lakini haisaidii, arejeshwe kazini naagiza apewe ulinzi wa kutosha.”

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Waziri Mkuu alisema zaidi ya Sh. milioni 600 hazijulikani zilipo, huku kiasi cha Sh. milioni 98.5 zikidaiwa kuingizwa katika akaunti za watumishi wa halmashauri hiyo bila maelezo yoyote.

Majaliwa amewataja watumishi hao ni Devid Onyango aliyechukua Sh. milioni 51, Elakada Kanongole Sh. milioni 36, Fork Karunde Sh. milioni nane na Charles Chali Sh. milioni 2.5.

Habari Kubwa