Lipumba awapa majukumu makatibu CUF uchaguzi mitaa

16Sep 2019
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lipumba awapa majukumu makatibu CUF uchaguzi mitaa

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimewapa majukumu watendaji wake kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba.

Watendaji hao ambao ni Makatibu wa Wilaya zote za Tanzania Bara, walipewa majukumu hayo jana, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, alipokuwa anafungua semina ya siku tatu  kwa  ajili ya kuwawezesha kujifunza mambo kadhaa.

Alisema jukumu la kwanza la makatibu hao ni  kubainisha majukumu na wajibu wa Makatibu wa Wilaya kwa mujibu wa Katiba ya CUF kwa mujibu wa Ibara ya 71.

Prof. Lipumba alisema Katibu wa Wilaya ndiye mtendaji mkuu wa chama katika wilaya anayepaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maamuzi ya vikao vya kikatiba na maelekezo ya Katiba ya Chama.

“Miongoni mwa majukumu hayo ni kutunza mali za chama, kutunza takwimu  za wilaya, kata na matawi yote yaliyomo ndani ya wilaya kuhusu wanachama, wapigakura kwenye kila mtaa, kijiji, kitongoji, kata na jimbo,” alisema.

Alisema semina hiyo itawawezesha makatibu kuyaelewa kadhaa ikiwamo katiba ya chama ili waelewe majukumu na wajibu wao na umuhimu wa ushirikiano na kuheshimu maamuzi ya vikao katika utendaji wa kila siku.

Mwenyekiti huyo alisema kipa kuielewa sera na itikadi ya CUF, Sera ya Haki Sawa kwa Wote na Itikadi ya Utajirisho kama ilivyofafanuliwa kwenye Utangulizi wa Katiba ya CUF kwenye Tamko la Waasisi wa Chama lililotolewa 1992 msingi wake mkuu ni tamko la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu.

Alisema itikadi ya utajirisho maana yake ni kutumia utajiri wa nchi kwa manufaa ya wananchi wote. “Hii ndiyo sababu tumekuwa tukipiga vita ufisadi nyakati zote kwa kuwa asili ya ufisadi ni kutumia utajiri wa nchi kwa maslahi ya mafisadi wachache,” alisema na kuongeza:

 

 “Utajirisho maana yake ni haki sawa kwa wote na neema kwa wote. Tunapozungumzia haki sawa kwa wote tunamaanisha haki ya kisiasa, haki za kiuchumi, haki za kijamii katika maisha yetu ya kila siku.”

Alisema lengo la semina hiyo ni kuwaanda makatibu wa wilaya kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji kwa kuangalia changamoto za kanuni na mwongozo wa uchaguzi.

Prof. Lipumba aliwatala  makatibu hao kuwa makini na njama za CCM na wasimamizi wa uchaguzi huo hasa kutokana na uzoefu wa uchaguzi uliopita ambapo wasimamizi wamekuwa wanawatangaza wagombea wa CCM kuwa wamepita bila kupingwa.

“Suala la wapigakura kutakiwa kuwa na vitambulisho ndio waweze kujiandikisha na hatimaye kupata fursa ya kupiga kura ni tatizo, na kwa hakika ni utaratibu unaopora haki za kisiasa kwa maana ya kupiga au kupigiwa kura,” alisema.

Alisema kama Rais alionyesha wasiwasi wake juu ya usajili wa line za simu kufanyika kwa kutumia vitambulisho vya Taifa kwa kuwa havijakamilika kwa Watanzania, basi hata vitambulisho vingine vilivyotajwa kuwa vitatumika kwenye uchaguzi huu wa mitaa vinakumbana na changamoto hiyo hiyo, na kwamba  kama hali ndio hiyo, basi wataoshiriki kwenye kuchagua viongozi wa serikali za mitaa watakuwa ni wachache sana.

Alisema CUF inamtaka Waziri wa Tamisemi kutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka kwa kuondosha vikwazo vinavyotishia kupunguza idadi ya wapigakura.

Prof. Lipumba aliitaka Tamisemi kuweka orodha ya mitaa, vijiji na vitongoji kwenye tovuti yake ili kurahisisha vyama vyenye uwezo wa kuchukua taarifa hizo na kuzifanyia kazi.

Habari Kubwa