Bunge laitaka serikali  kutumia vifaa vya polisi

16Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Bunge laitaka serikali  kutumia vifaa vya polisi

BUNGE limeitaka serikali kuvitumia vifaa vya Jeshi la Polisi ambavyo vipo kwenye makontena bandarini kama taratibu zinavyoelekeza.

Spika wa Bunge Job Ndugai.

Hatua hiyo imekuja baada ya wajumbe wa kamati mbili walioteuliwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kufuatilia suala la vifaa hivyo kutokana na kuwapo kwa mjadala baadhi ya wabunge kudai kuwa vifaa hivyo havijanunuliwa na Kampuni ya Daissy General Traders iliyopewa zabuni hiyo.

Akizungumzia suala hilo mwishoni mwa wiki wakati akiahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge, Spika Ndugai alisema wakati wa Bunge la Bajeti siku ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi liliibuliwa suala la vifaa hivyo, huku Waziri Lugola akisisitiza vifaa hivyo vipo.

“Wakati Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, anahitimisha hoja yake kulikuwa na suala la vifaa vya Jeshi la Polisi ambavyo ilikuwa inadaiwa kwamba havijanunuliwa wengine wanasema vimenunuliwa na Waziri alishuhudia hapa bungeni kuwa vifaa vipo,” alisema.

Alifafanua kuwa baada ya hoja hiyo aliteua wajumbe kadhaa wa Kamati za Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), ambapo walienda wajumbe wakashuhudia makontena hayo yaliyopo bandarini yana vifaa.

“Walikuta makontena yapo yakafunguliwa wakaona vifaa vipo na kwa vile jambo hili ni la muda mrefu na vifaa vipo na jeshi linahitaji vifaa vile kwa niaba ya Bunge, serikali kwa kweli endeleeni kuvitumia hivyo vifaa kama taratibu zenu zinavyoelekeza,” alisema.

Alieleza kuwa “Kwa sababu sisi kama Bunge tumeshajiridhisha vifaa vile vipo mambo mengine kiutaratibu yatafuata kama kawaida, lakini sisi Bunge tunasema endeleeni tumieni vifaa hivyo kwa kuwa vipo ni vingi na hakuna sababu ya kuagiza vingine wakati hivyo vipo vimeshagharamikiwa.”

Mkutano wa Bunge wa 15, sakata la vifaa hivyo liliibuliwa bungeni wakati wa Bunge la Bajeti hali iliyomlazimu Spika kuteua wajumbe wa kamati hizo kufuatilia suala hilo.

Katika mkutano huo, ilidaiwa kuwa Kampuni ya Daissy General Traders ambayo inamilikiwa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Angela Kizigha, ilipewa zabuni ya kuleta kofia, sare na makoti ya mvua lakini haijawasilisha licha ya kulipwa fedha huku wengine wakisema vimeletwa lakini ni feki jambo ambalo Bunge limejiridhisha na kuagiza vitumike.

Habari Kubwa