Bil. 10/- kujenga hospitali mkoa

16Sep 2019
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Bil. 10/- kujenga hospitali mkoa

UJENZI wa hospitali ya rufani ya mkoa wa Singida unaoendelea kwenye eneo la Mandewa, Manispaa ya Singida, utagharimu Sh. bilioni 10, badala ya Sh. bilioni 150, zilizokusudiwa awali kabla ya serikali kuingia madarakani mwaka 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alisema hayo jana baada ya   Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Deogratius Banuba, kusoma risala mbele ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye makabidhiano ya gari la kubebea wagonjwa, lilitolewa Mbunge Viti Maalumu (CCM), Aysharose Mattembe.

Katika risala hiyo, Dk. Banuba ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji mifupa, alisema kasi ya mradi huo inakabiliwa na changamoto ya fedha ili kukamilika kama ulivyokusudiwa kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 125, kutoka lile la awali dogo lililopo katikati ya mji wa Singida.

Dk. Banuba alisema licha ya fedha hizo kutumika kwa ajili ya majengo yote yenye hadhi ya hospitali ya rufani katika eneo hilo, pia zitagharamia nyumba za madaktari, vifaa tiba, ujenzi wa nyumba za wataalamu wengine wa afya, chuo cha madaktari na huduma nyinginezo za tiba.

Msaada huo kutoka kwa Mbunge Mattembe unajumuisha vitanda 16, vikiwamo saba vya kulalia wagonjwa na viwili vya wajawazito kujifungulia vikiwa na thamani ya Sh. milioni 14, na gari la kisasa la kubebea wagonjwa lenye muundo wa Hiace, lenye thamani ya Sh. milioni 21.

Akifafanua juu ya fedha hizo, Dk. Nchimbi alisema haiwezekani kiasi chote hicho kigharamie mradi huo, wakati hivi sasa serikali imeshajenga hospitali mpya mbili katika wilaya ya Mkalama na Halmashauri ya Wilaya ya Singida kwa Sh. bilioni tatu tu.

"Gharama hizi ni kubwa, tumejenga hospitali mbili kwa Sh. bilioni tatu, Sh. bilioni 1.5 Mkalama na Sh. bilioni 1.5 zingine Singida Vijijini na zote zimekamilika. Hii  hospitali ya rufani tunataka itumie Sh. bilioni 10 tu,” alisema.

Akizungumza na waganga, wauguzi, watumishi wa hospitali hiyo na wananchi kwa ujumla, Dk. Tulia alipongeza juhudi za Mattembe katika kuisaidia jamii ya Singida, hususan sekta ya afya.

Alisema alichokifanya Mattembe kinapaswa kupongezwa kwa kuwa fedha alizotumia kununulia vifaa hivyo angeweza kutumia kwa matumizi binafsi, lakini kutokana na upendo alio nao kwa wananchi wake, ameona vyema azielekeze kwenye huduma ya afya.

Awali Mattembe alisema kuwa amelazimika kutoa msaada huo kutokana na hospitali hiyo ya rufani kukosa gari la kubebea wagonjwa, hali iliyoathiri ufanisi wa kuwahudumia wagonjwa hasa wajawazito wanaozidiwa na uchungu wanapokwenda kujifungua.

Ujenzi wa hospitali ya rufani ya mkoa wa Singida, ulianza kutekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa usimamizi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa Dk. Parseko Kone, lakini hadi sasa mradi huo mkubwa kabisa haujakamilika.

Habari Kubwa