Malaria kuwa historia 2030

16Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Malaria kuwa historia 2030

WAKATI ugonjwa wa malaria ukitajwa kuongoza kwa vifo duniani, wabunge wa Tanzania walioko kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo, wametoa kauli ya matumaini kuwa hadi kufikia mwaka 2030 tatizo hilo litakuwa limetokomezwa kabisa.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainab Chaula.

Kauli hiyo ya kuleta matumaini ilitolewa juzi na Umoja wa Wabunge walio katika vita dhidi ya malaria na Magonjwa ya Ukanda wa Joto Yasiyopewa Kipaumbele (Tapama), kupitia Katibu wake, Dk. Raphael Chegeni, wakati akikabidhi mpango mkakati wa kutokomeza malaria nchini kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainab Chaula.

Katika semina hiyo ya siku mbili iliyofanyika mwishoni mwa wiki, iliyojumuisha wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya malaria, Dk. Chegeni alisema wameanza juhudi ya utekelezaji wa mpango wa kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Dk. Chegeni alisema mpango mkakati huo unalenga kuwakumbusha wabunge kuwajibika katika kujua takwimu za vifo na wagonjwa walioko kwenye majimbo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tapama, Riziki Lulida, alisema wameandaa mpango mkakati huo baada ya kuona vifo vingi kwa wajawazito na watoto waliopo chini ya miaka mitano.

"Tulikaa chini tukaona hakika tunapoteza kizazi kinachotegemewa hapo baadaye hasa katika mikoa ya minne yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huu ambayo Kigoma, Geita, Kagera, Lindi na Mtwara," alisema Lulida.

Naye Mwenyekiti wa Marais Wastaafu na Viongozi wa Juu wa Afrika wa (Alma), Joyce Kasonabo, alisema malengo ya Alma ni kuweka kipaumbele kwa ugonjwa huo wa malaria unatokomezwa kisera na kimataifa.

Alisema ugonjwa huo hauwezi kutokomezwa na mtu mmoja mmoja, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainabu Chaula, akipokea mpango huo wa kutokomeza malaria alisema kila mmoja ana nafasi yake kuhakikisha anatokomeza ugonjwa huo.

Alisema ugonjwa huo upo na umekuwa tishio kwa kuua nguvu kazi ya taifa. Aliongeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya imefanikiwa kutokomeza ugonjwa huo kutoka asilimia 14.4 mpaka asilimia 7.3.

Habari Kubwa