Pigeni kura ili Mlima K'njaro uwe kivutio bora duniani

16Sep 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Pigeni kura ili Mlima K'njaro uwe kivutio bora duniani

MLIMA Kilimanjaro umeingia katika shindano la kimataifa la kuwania tuzo za dunia za kivutio bora zaidi cha utalii kinachoongoza kwa mwaka 2019.

Tuzo hizo za World Travel Awards, zimeuweka mlima huo kwenye orodha ya nchi bora zenye vivutio adimu Afrika na duniani.

Jana, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Uhifadhi nchini (SAC), Paschal Shelutete, aliithibitishia Nipashe kuwa kazi ya kupiga kura kwa njia ya mtandao ilianza rasmi Septemba 12 na inatarajiwa kufikia ukomo Oktoba 20 mwaka huu.

"Tunawaomba Watanzania kuupigia kwa wingi kura Mlima Kilimanjaro ambao umeingia tena katika shindano la kimataifa la kutafuta kivutio bora zaidi cha utalii kinachoongoza duniani kwa mwaka 2019.

"Kura zote zinapigwa kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya worldtravelawards.com/vote kwa kusajili taarifa zako na kuingia rasmi katika mfumo wa upigaji kura."

Kura zitakazopigwa, ndizo zitakazoamua mshindi kutokana na wingi wa kura ambazo Mlima Kilimanjaro itapata.

Aidha, taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya World Travel Awards inaonyesha kuwa utaratibu kama huo ulifanyika Mashariki ya Kati, Februari mwaka huu, wakati Ulaya pazia hilo lilifunguliwa Machi 11 mwaka huu.

Pia, zilionyesha kuwa Amerika ya Kati, Amerika ya Kusini na Asia, pazia hilo lilifunguliwa Machi 25 mwaka huu.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2013, Mlima Kilimanjaro ulishinda tuzo ya maajabu saba ya asili ya Afrika na kuipa Tanzania heshima kubwa kutokana na kuwa na kivutio hicho cha kipekee cha utalii.

Mlima Kilimanjaro ni miongoni mwa hifadhi tano zilizopo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), ambazo zinaoongoza nchini kwa mapato na kuziendesha hifadhi nyingine.

Habari Kubwa