Mzee Mugabe; Mpigania uhuru aliyekumbukwa kabla hajafa

18Sep 2019
Mashaka Mgeta
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mzee Mugabe; Mpigania uhuru aliyekumbukwa kabla hajafa

HABARI zake bado zinaendelea kuandikwa, historia yake inaelezewa kabla ya mwili wake kuzikwa katika siku ambayo haijatangazwa rasmi.

Waombolezaji wakiwa na bango lenye picha ya Robert Mugabe siku ya kuaga mwili wake jijini Harare nchini Zimbabwe.

Mpigania uhuru wa Afrika aliyeiongoza Zimbabwe tangu mwaka 1987 hadi 2017, Robert Gabriel Mugabe, alifariki dunia Septemba 6, mwaka huu kwenye Hospitali ya Gleneagles nchini Singapore, alikokuwa akitibiwa.

Mugabe amefariki akiwa na miaka 95 huku akikumbukwa kwa ujasiri wake dhidi ya ukoloni kutokana na misimamo yake nchini Zimbabwe.

Wanaofuatilia na ‘kuziishi’ fikra za ki-Magharibi, wanamuona Mugabe kama kiongozi mwenye hulka ya udikteta, kwa namna alivyoitawala nchi hiyo kwa takribani miaka 37.

Lakini barani Afrika na hasa wanaojua na kuifuatilia historia ya ukombozi uliojikita katika kudai uhuru, haki, usawa na hadhi ya ‘mtu, Mugabe anaangaziwa kama jemedari wa vita aliyevishinda vikosi vyenye silaha kubwa na nguvu za kijeshi, akabaki kuwa mshindi.

Kwa sababu ya wigo mpana wa mawasiliano, mikakati ya kueneza propaganda, japo kutaja kwa uchache, sifa hasi dhidi ya Mugabe zilienea kwa kasi na hivyo kuyafanya mambo mema aliyolitendea taifa lake na raia wa Zimbabwe kutojulikana.

KUTETEA UHURU

WA ZIMBABWE

Mugabe aliuamini na kuutetea uhuru wa Zimbabwe uliopatikana 18 Aprili 1980, na mara kadhaa alipenda kuweka bayana kwamba uhuru huo na ule wa raia wake ni mambo yanayopaswa kuheshimiwa daima.

Aliyasema hayo wakati akijibu mashambulizi ya propaganda zilizoenezwa na mahasimu wake wa kisiasa na utawala, hasa nchi za Magharibi.

Mugabe alisimamia msingi wa kuzirejesha rasilimali za raia wa Zimbabwe na hasa ardhi kuwa milki ya Wazimbabwe, akisisitiza kwamba si raia wa nchi hiyo tu, bali hakuna mwafrika aliyewahi kwenda kudai na kumiliki ardhi kwa nguvu kwenye mataifa hayo (Magharibi) kama wanavyofanya baadhi ya raia wao kwa Afrika.

Moja ya kauli yake iliyowahi kuzua mjadala mkubwa ni pale alipowahi kutamka, “Sisi sio watu wa Ulaya, hatujawahi kuomba hata sehemu ndogo ya Ulaya, Blair, kaa na Uingereza yako na mimi niache nibaki na Zimbabwe yangu.”

Tony Blair alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kuanzia mwaka 1997 to 2007. Pia Blair alikuwa kiongozi wa chama cha Labour kuanzia 1994 hadi 2007. Aliwahi kuwa kiongozi wa upinzani kuanzia 1994 mpaka 1997 na kati ya 1983 na 2007, Blair alikuwa mbunge wa jimbo la Sedgefield.

Historia inamuangazia Mugabe hasa yanapotajwa masuala ya ardhi yaliyosababisha kuporomoka kwa uhusiano kati yake na wakulima wakubwa wa kizungu.

Wakati wa mzozo wa ardhi uliosababisha ghasia nchini humo, Mugabe aliwahi kutamka, “Hii ni ardhi ya mtu mweusi, hivyo ni mtu mweusi ndio ana haki ya kuamua nani akae na nani asikae. Tuna ardhi yetu na katika ardhi yetu ndio tutapata fedha.”

Kwa upande mwingine, yapo mafanikio kadhaa aliyoyafikia Mugabe katika kipindi cha utawala wake.

Miongoni mwa sekta zilizoboreka, kukua na kuwa mfano bora kwa kiongozi huyo alipokuwapo madarakani ni afya na elimu kwa weusi walio wengi dhidi ya wazungu wachache waliokuwa wanufaika wakubwa baada ya uhuru.

KUMINYA UPINZANI

Licha ya mafanikio yake katika maendeleo ya nchi na ustawi wa raia wa Zimbabwe, Mugabe alikosolewa kwa namna alivyowadhibiti wapinzani na shughuli zao za kisiasa, akitumia zaidi majeshi ya taifa hilo lililopo Kusini mwa Afrika.

Majeshi hayo yalionekana tena katika utekelezaji wa kunyakuwa ardhi kutoka kwa wakulima wachache wa kizungu, hatua iliyomfanya kuzidi kuungwa mkono na wapigakura wa nchi hiyo huku akichukiwa na washirika wa maendeleo kimataifa.

SAFARI YA KUONDOKA MADARAKANI

Dalili za Mugabe kuelewa na ‘mzigo’ wa urais zilianza kuonekana baada ya kuibuka kwa mzozo kati yake na aliyekuwa Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa ambaye kwa sasa ndiye Rais wa nchi hiyo.

Ingawa mzozo huo ulikua kiasi cha kusababisha Mugabe ‘kuwekwa kizuizini’ na baadaye kuondolewa madarakani, wahusika wa mpango huo wakitajwa kuwa washirika wa Mnangagwa, Rais huyo wa sasa wa Zimbabwe akafunguka kusifu na kupongeza utawala wa Mugabe, baada ya habari za kifo chake kuenea kuanzia nchini humo hadi pande zote za dunia.

Kwa Mnangagwa, hadi kuwa shujaa wa taifa kama alivyokabidhiwa na chama chake cha Zanu –PF, ilimstahili Mugabe.

KUKUMBUKWA KWAKE

Ingawa Mugabe anatajwa kwa mema mengi baada ya kufariki dunia, lakini zipo taarifa kuwa raia wa Zimbabwe walianza kumtaja kwa utawala wenye mafanikio, siku kadhaa baada ya kuondolewa madarakani, yaani kabla ya kifo chake.

Raia kadhaa wa Zimbabwe walikaririwa wakisema licha ya ugumu wa maisha waliyokuwa nayo wakati wa utawala wa Mugabe, lakini uongozi wa Mnangagwa ulisababisha hali kuwa ngumu zaidi.

Miongoni mwa wananchi waliokaririwa wakilalamikia ugumu wa maisha baada ya Mugabe kuondolewa madarakani ni pamoja na Fadzayi Mahere wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC).

Chama cha MDC kikiongozwa na Morgan Tsvangirai aliyefariki Februari 14, mwaka jana huko Johannesburg, Afrika Kusini kiligawana mamlaka ya utawala na Mugabe baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2008, ulioghubikwa na vurugu na madai ya wizi wa kura uliofanywa na watawala.

Ili kurejesha hali ya utulivu na amani nchini humo, iliundwa serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyosababisha kuwapo mgawanyo wa madaraka, Tsvangerai wa MDC akawa Waziri Mkuu.

Ni kutokana na hali ngumu ya maisha, upinzani nchini humo ukikihusisha chama cha MDC, kikatoa rai kwa Wazimbabwe kuandamana, ikiwa ni ishara ya kupinga hali ngumu ya maisha kiuchumi.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya Mugabe kundolewa madarakani 2017 na taifa hilo kuwa chini ya uongozi wa Mnangagwa.

Kigezo kikubwa kilichotumiwa kutathmini hali ya maisha ya watu ni viashiria vya uchumi vilivyoyagusa maisha ya raia wa Zimbabwe, miongoni mwao vikiwa ni ufinyu wa ajira, kushuka kwa kipato ikiwamo mishahara na kudorora kwa biashara.

HISTORIA FUPI

Mwaka 1980, Mugabe alishinda uchaguzi na kuwa Waziri Mkuu.

Mwaka 1982 aliushutumu upinzani kwa kupanga njama za kutaka kuipindua serikali yake.

Mwaka 1987, utawala wa Mugabe ulibadilisha Katiba ili imruhusu kuwa Rais na kuongeza mamlaka yake.