NACTE wafungua udahili wa mwisho

18Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
NACTE wafungua udahili wa mwisho

BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) limesema linaendelea na udahili kwenye taasisi na vyuo vyote vilivyosajiliwa au kuwa na programu zinazotambuliwa na baraza kutoa mafunzo ngazi ya astashahada na stashahada.

Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa baraza (Nacte), Twaha Twaha

Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa baraza hilo, Twaha Twaha, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema pia wanaendelea kufanya uhakiki wa majina 58,193 ya waliochaguliwa na taasisi na vyuo mbalimbali vinavyotoa elimu ya ufundi na mafunzo.

Alisema majibu ya uhakiki yatatolewa Oktoba 4, mwaka huu, kama ilivyo kwenye kalenda ya baraza inayoongoza shughuli za kitaaluma.

“Kwa kuzingatia kuwa bado kuna vyuo vyenye nafasi wazi na kwamba wapo wanafunzi ambao hawajadahiliwa kwenye chuo na taasisi yoyote lakini wanayo nia ya kufanya hivyo, Nacte ilifungua dirisha la udahili kwa awamu ya pili na ya mwisho kwenye vyuo na taasisi zinazotoa programu za astashahada na stashahada nchini kuanzia Septemba 7, mwaka huu na litafungwa Septemba 25," Twaha alisema.

Aliongeza kuwa nafasi za kujiunga na vyuo vya ualimu na uuguzi vya serikali zimejaa na hivyo wanaendelea kudahiliwa kwa vyuo vingine.

Twaha pia aliwataka wahitimu wa kidato cha nne na sita na walio na sifa za kujiunga na programu mbalimbali, kutumia fursa hiyo kutuma maombi ya udahili kwenye taasisi na vyuo vyenye nafasi na ambavyo bado vinapokea maombi au udahili katika ngazi ya astashahada na stashahada.

Alisema majina ya watakaochaguliwa na taasisi na vyuo mbalimbali yatawasilishwa Nacte kuanzia Septemba 25 hadi Septemba 27, mwaka huu kwa ajili ya uhakiki.

Mbali na hilo, Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (Tahliso), ilifanya ziara ya mafunzo Nacte kwa lengo la kupata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu taasisi hiyo na namna inavyofanya kazi.

Mwenyekiti Tahliso, Peter Niboye, akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, aliwataka wanafunzi kutimiza wajibu wao ikiwamo kutembelea tovuti ya Nacte yenye mifumbo mbalimbali itakayowawezesha kutatua changamoto zao kwa wakati bila kufika ofisini.

“Pia kama Tahliso tunavitaka vyuo kudahili kwa kufuata kanuni na vigezo walivyoelekezwa na Nacte na hii ikiwa ni pamoja na kufuata mitaala kama inavyoelekezwa ili kuzalisha wataalamu walio bora,” Niboye alisema.Kiongozi huyo wa Tahliso pia aliitaka serikali na vyuo kuimarishe ulinzi na usalama katika vyuo ili wanafunzi waishi kwenye mazingira salama.