6 mbaroni tuhuma kutakatisha bil. 4/-

18Sep 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
6 mbaroni tuhuma kutakatisha bil. 4/-

WATU sita wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kuratibu genge la ujangili, kukutwa na nyara za serikali na kutakatisha zaidi ya Sh. bilioni nne.

Washtakiwa hao ni Hassan Likwena (39) maarufu Nyoni,  Bushiri Likwena, Oliver Mchuwa (35), Salama Mshamu (21), Haidary Sharifu (44), maarufu White na Joyce Thomas (33).

Washtakiwa hao wote walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Mawakili wa Serikali Salim Msemo, Tully Helela na Elizabeth Mkunde.

Wankyo alidai shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanatuhumiwa kwa kushiriki genge la uhalifu kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 3, mwaka huu katika mikoa ya Mtwara, Pwani na Dar es Salaam, kupanga uhalifu wa kupokea vipande vya meno ya tembo na kiboko.

Shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Septemba 3, mwaka huu eneo la Saku, Chamazi, walikutwa na meno ya tembo  413 yenye thamani ya Dola za Marekani 1,755,000 bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la pili, washtakiwa walikutwa na vipande viwili vya meno ya kiboko vikiwa na thamani ya Dola za Marekani, 1,500 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2017 na Septemba 3,mwaka huu, washtakiwa walitakatisha Sh. 4,043,463,000 na kukutwa na nyara hizo za serikali wakati wakijua ni zao la kosa tangulizi la ujangili.

Hata hivyo, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote mpaka upelelezi utakapokamilika na kuhamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Oktoba Mosi, mwaka huu na washtakiwa watarudishwa mahabusu.

Habari Kubwa