Azam kuiwahi mapema Triangle kwa mafungu

18Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Azam kuiwahi mapema Triangle kwa mafungu

HUKU wakiwa na deni la bao 1-0 waliloruhusu katika mechi yao ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano hiyo, Azam FC wataifuata mapema Triangle FC lakini kwa mafungu.

Katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo iliyopigwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, Azam ilikubali kipigo hicho licha ya kumiliki mpira kwa kipindi chote, hivyo inahitaji kushinda kuanzia mabao mawili ili kuweza kusonga mbele.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, juzi, Ofisa Habari wa Azam FC, Jafari Maganga, alisema Kocha Mkuu  wa kikosi hicho, Mrundi Etienne Ndayiragije, ameshauri waende Zimbabwe mapema ili kuweza kuzoea hali ya hewa na mazingira ya watakapocheza mechi hiyo.

"Kutokana na ushauri huo wa kocha, tutaelekea Zimbabwe Septemba 22 kabla ya mechi hiyo ambayo imepangwa kuchezwa Septemba 28, mwaka huu," alisema.

Aidha, alisema kutokana na baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho kukabiliwa na majukumu ya timu ya Taifa, Taifa Stars ambayo ipo kambini kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) dhidi ya Sudan, wataondoka kwa mafungu mawili.

"Kundi la kwanza litaelekea Zimbabwe Septemba 22 kabla ya wachezaji waliopo Stars pamoja na kocha mkuu kuungana na wenzao nchini humo siku moja baadaye," alieleza.

Hata hivyo, Ndayiragije ambaye anakaimu nafasi ya kocha mkuu katika kikosi cha Stars, ameeleza Azam FC inaweza kupindua matokeo hayo kwa kuwa ameshafahamu uchezaji wa wapinzani wao na kuanza kufanyia marekebisho makosa yaliyojitokeza awali.

"Tatizo kubwa wapinzani wetu [Triangle FC], walicheza bila kufunguka na kufanikiwa kupata bao ambalo waliweza kulilinda hadi mpira unamalizika," Ndayiragije alisema.

"Wengi wanaamini kwamba ushindi ni nyumbani, lakini hata ugenini unaweza kupata matokeo kama ilivyokuwa wao na nimewaeleza wachezaji wangu tunaweza kushinda ugenini."

Habari Kubwa