Wazazi mshindi mil. 825/- za SportPesa wafunguka

18Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wazazi mshindi mil. 825/- za SportPesa wafunguka

BAADA ya mwanawe kuwa mmoja kati ya washindi wawili waliojishindia jumla ya Sh. milioni 825.9 kupitia Jackpot ya Sportpesa mwezi uliopita, baba mzazi wa Magabe Marwa, Marwa Maratho, amefunguka kuhusu ushindi huo.

Mshindi wa Jackpot ya Sh. milioni 825, Magabe Marwa, akiwa na familia yake. Kulia ni baba yake, Marwa Maratho, wapili kushoto ni mama yake,Wisiko Warioba akifuatiwa na mke wa mshindi, Elizabeth Wambura.

Magabe na mwenzake Kingsley Pascal kutoka Biharamuro, Kagera mwezi uliopita walifanikiwa kushinda kwa pamoja mamilioni hayo kabla ya kugawana na kila mmoja kuibuka na Sh. milioni 412 kufuatia kutabiri kwa usahihi mechi 13 za Jackpot.

Akifungukia ushindi huo wa mwanawe, Maratho alisema  hakuamini wakati anampigia simu akimtaarifu ushindi wake akiwa anachunga mifugo yake.

“Wakati ananipigia simu kunitaarifu sikuamini, nilikuwa nachunga lakini alipokuja kunipigia binamu yake ambaye ni mkuu wa wilaya na kunitaarifu kwamba kijana wangu ameshinda na SportPesa, hapo ndio moyo ukaanza kufarijika kwamba na mimi nimeingia kwenye utajiri usiotarajiwa.

“Nilijisikia vizuri kabisa na jasho lilinitoka sehemu zote, ushauri wangu kama baba yake asikurupukie kufanya vitu. Aendelee na kazi yake, hizo hela aziweke na baada ya hapo tutakaa baadaye mimi na mama yake tutatafuta ushauri.

“Mimi sifa ambayo napenda aendelee nayo ni utanashati na upendo kwa watu maana bila upendo hata uwe na pesa ni bure, napenda kuwashukuru SportPesa, pia namuombea kijana wangu aitumie hiyo pesa vizuri na imsaidie yeye na ukoo wetu wote bila ubinafsi.

HUYU HAPA MAMA YAKE

Wisiko Waryoba ambaye ni mama wa Magabe, alisema: “Nilikuwa nyumbani nakamua maziwa ndio nikapata simu ya Magabe kuwa ameshinda mamilioni. Kwa kweli nilijisikia vizuri kwa sababu mtoto ameshinda na atanikomboa na maisha yangu magumu niliyoanza nayo.

“Awe ni mtoto mwenye imani na ningemshauri akae kwanza atulie kidogo na ndipo baadaye apange jinsi ya kuzitumia fedha hizo ambazo ni nyingi kwa kweli.

“Kwa ujumla fedha hizo zitatumika kifamilia kwa sababu hiyo hela aliyoshinda itasaidia kutatua changamoto ya maisha tuliyoanza nayo yasiweze kujirudia.

“Nilikuwa sina nyumba ya kuishi kwa hiyo mtoto wangu ameshinda hela hivyo nitapata nyumba ya kuishi na pia nitaendelea kuishi maisha mazuri."

Habari Kubwa