Vita Simba vyaanza, Mexime macho kodo

18Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vita Simba vyaanza, Mexime macho kodo
  • *** Apania kubeba tena pointi zote msimu huu huku Aussems akieleza ugumu uliopo wakati ushindani wa namba ukizidi...

WAKATI Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime akiendelea kutolea tena 'macho kodo' pointi sita za Simba, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, safu yake ya ushambuliaji imezidi kunoga baada ya vita vya ushindani wa namba kuongezeka kufuatia kurejea kwa Mbrazil Wilker da Silva aliyekuwa majeruhi.

Msimu uliopita, Kagera Sugar ikiwa katika Uwanja wake wa Kaitaba mjini Bukoba, iliichapa Simba kwa mabao 2-1 kabla ya kuja Uwanja wa Taifa na kuondoka tena na pointi tatu kufuatia kuitandika bao 1-0.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa Simba ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili dhidi ya JKT Tanzania mabao 3-1 na kisha kuichapa Mtibwa Sugar 2-1, Kagera Sugar nayo mambo ni moto.

'Wakulima wa Miwa' hao, nao wameshinda mechi mbili huku milango yake ikiwa migumu hadi sasa kufuatia kushinda 2-0 dhidi ya Biashara United na kisha kuichapa Alliance FC bao 1-0, jambo ambalo Mexime anaamini kikosi chake ni bora msimu huu na kinaweza kuendeleza rekodi yake ya kuifunga Simba.

Mexime amesema anaamini Septemba 26, mwaka huu watakapokutana na Simba katika Uwanja wa Kaitaba, wanaweza kuwafunga tena mabingwa hao watetezi licha ya kuundwa na mastaa wengi wa kigeni.

Hata hivyo, kwa upande wa Simba inazidi kuimarika kufuatia winga wao Miraji Athumani kuandaliwa kuwa 'supa sab' na tayari amefunga katika mechi zote mbili akitokea benchi.

Lakini mbali na Miraji, kurejea kwa mshambuliaji Mbrazil Da Silva kumerejesha matumaini makubwa katika kikosi hicho ambacho bado kina hazina ya wachezaji wengi kwenye benchi lake, akiwamo Ibrahim Ajibu, suala ambalo linaelezwa litaamsha ushindani mkubwa wa namba.

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, akizungumza na Nipashe jana baada ya mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, alisema hali ya wachezaji wake kwa ujumla sasa ni nzuri na kikosi kinazidi kuimarika kila uchao licha ya nahodha wao, John Bocco kuwa mchezaji pekee aliyeko nje akiendelea kuuguza majeraha ya mguu.

"Wachezaji wanaendelea vizuri makosa machache ambayo nimeyaona kwenye mchezo uliopita naendelea kuyafanyia kazi ili yasijirudie tena," alisema Aussems ambaye anatambua vema ugumu wa mechi ijayo dhidi ya Kagera Sugar.

Alisema mchezo ujao unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani na kuahidi kutumia nguvu nyingi kwa wachezaji kuhakikisha wanatetea ubingwa wao.

"Sasa hivi nguvu zangu zote naziweka kwenye Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA ili kuiweka mahali pazuri timu yangu naomba Wanasimba wazidi kutusapoti," alisema.

Kwa upande wa Meneja wa kikosi hicho, Patrick Rweyemamu alisema anashukuru kikosi kinaendelea vizuri kwa ajili ya mchezo huo.

"Sisi kwetu kila mechi ni fainali hatutaki kupoteza mchezo hata mmoja," alisema.

Habari Kubwa