Yanga wajichimbia Dar kuijadili Zesco

18Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga wajichimbia Dar kuijadili Zesco

YANGA imeanza mpango mkakati wa kuhakikisha inaitoa Zesco na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya mwishoni mwa wiki kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa hivyo kuwa na deni kubwa la kulipa bao hilo la ugenini.

Na ili kuhakikisha wanafanya kama ilivyokuwa dhidi ya Township Rollers ugenini Botswana, leo uongozi wa klabu hiyo umepanga kujichimbia katika kikao kizito cha kuandaa mkakati wa ushindi.

Tayari Yanga ilishaeleza kuwa itawasili nchini Zambia wiki moja kabla ya mechi ili kuyasoma vema mazingira na kuzoea hali ya hewa ya huko, lakini leo watajadili mkakati mzito wa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na hatimaye kupata ushindi.

"Hicho kikao kitakuwa na mikakati binafsi ambayo watu hawatakiwi kuifahamu kwa sababu kwenye mpira kuna mambo mengi ambayo mengine yanafanywa kisirisiri," kilisema chanzo chetu ndani ya klabu hiyo ambacho kiliomba hifadhi ya jina lake.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hamad Islam aliwataka Watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo yaliyopita na badala yake wazidi kushikamana mpaka mwisho.

Mjumbe huyo alisema, lengo lao ni kuhakikisha timu yao inakwenda kufanya vizuri ugenini na kurudi na matokeo mazuri nyumbani na suala la kuitupa nje Zesco United linawezekana kama walivyoifanyia Township Rollers mjini Gaborone.

Katika mechi ya raundi ya awali ya michuano hiyo, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa dhidi ya Township Rollers kabla ya kwenda Botswana na kushinda bao 1-0, matokeo ambayo pia wiki iliyopita waliyapata dhidi ya Zesco Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa