Wasichana 100 wasio na uwezo wapata ufadhili kidato cha tano

18Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
TUDARCO
Nipashe
Wasichana 100 wasio na uwezo wapata ufadhili kidato cha tano

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kushirikiana na Balozi wa Falme za Kiarabu, Khalifa Abdul-Ragman Al-Marzoo, wametoa ufadhili wa masomo kwa wasichana 100 wasio na uwezo waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kushoto), akizungumza na wanafunzi wa shule mbalimbali katika hafla ya kukabidhi msaada wa kimasomo kwa wanafunzi wa kike 100 waliofaulu masomo ya sayansi na kuchaguliwa kujiunga kidato cha tano kwa mwaka 2019, iliyofanyika jijini humo jana. Kushoto ni Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu hapa nchini, Khalifa Abdulrahman Mohammed Al Marzooqi.

Kati ya wanafunzi hao 75 ni waliofaulu masomo ya Sayansi na 25 ya Sanaa kutoka katika manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makonda aliomba msaada kwa balozi huyo ambaye alikubaliana na wazo lake la kuwasomesha wanafunzi hao 100 wa mkoa huo.

"Rais Magufuli amejitahidi kutoa elimu bure kwa wanafunzi hawa wa shule za msingi hadi sekondari kwa kutambua mchango wanafunzi wa kike ambao wanafaulu vizuri, lakini wazazi au ndugu zao hawana uwezo wa kuwasomesha, nimejitolea kuwatafutia ufadhili wa masomo," Makonda alisema.

Aliahidi kuwa wanafunzi hao atawasomesha hadi kidato cha sita na kila mwaka ataendelea kujitolea kuwatafutia ufadhili wanafunzi wengine.

Kwa upande wake, Balozi Al-Marzoo, alimpongeza Makonda kwa juhudi zake za kusaidia watoto wa kike wa masomo ya Sayansi ili kupata elimu.

Alisema Falme za Kiarabu zinashirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya kusaidia jamii ikiwamo ufadhili wa masomo.

Alisema amependa kusaidia wasichana hao 100 ambao wamefaulu kidato cha nne na hawana uwezo wa kuendelea na masomo kwa sababu anaamini wakipata elimu watakuja kusaidia jamii.

Alisema pia ameandaa ripoti kwa ajili ya kuomba miradi ikabidhiwe ofisini kwake badala ya kuwa chini ya madiwani kama ilivyo sasa.

Alisema madiwani wamekuwa wakikwamisha miradi ya maendeleo bila sababu.

"Wapo watendaji ambao wamekaa muda mrefu na kuchelewesha miradi mbalimbali kwa makusudi tu hayo majina yao tunayo na tunawafahamu na wengine wapo humu ndani," Makonda alisema.

Makonda pia alisema kabla ya kukubaliwa kwa ombi lake la miradi kupitishwa katika ofisi yake, hataacha kuwachukulia hatua watendaji watakaokuwa vikwazo katika kukwamisha miradi ya serikali.

"Tunaiandaa kamati ambayo itafuatilia mienendo ya miradi kila hatua ili tupate kujua nani anayekwamisha maendeleo na miradi ya serikali kwa sababu zake binafsi," alisema.

Habari Kubwa