Taboa yaipa jukumu Latra kutatua kero za wasafirishaji

18Sep 2019
Juster Prudence
TUDArCO
Nipashe
Taboa yaipa jukumu Latra kutatua kero za wasafirishaji

CHAMA cha wamiliki wa Mabasi (Taboa), kimesema ni vyema Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), kujikita kutatua kero za wasafirishaji na usafirishaji kwa ujumla kabla ya kuongeza jukumu la kukusanya mapato.

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu.

Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa mkutano kati ya wadau hao kujadili kanuni za sheria ya usafirishaji.

Alisema kuna kero nyingi katika sekta ya usafirishaji ikiwemo tozo mbalimbali ambazo siyo rafiki kwao hivyo aliwaomba Latra wafute tozo hizo ili kodi ibaki kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tunawaomba Latra wabaki kwenye jukumu lao la kutoa leseni na siyo kukusanya mapato ya faini mbalimbali kama wanavyotaka kufanya. Hatuna mgogoro na ukataji tiketi kwa mtandao wanachohitaji ni utaratibu kufuatwa,” alisema.

Naye, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Johansen Kahatano, aliwatoa wasiwasi wamiliki wa mabasi kwa kuahidi kutatua kero mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za usafirishaji.

Aidha, wamiliki wa mabasi kupokea sheria mpya zilizowekwa wakati jitihada za kupata utaratibu mpya ukiendelea.

Kwa mujibu wa Kahatano, Bunge ndio chombo chenye mamlaka ya kufanyia kazi maoni waliyotoa pamoja na wizara husika ambayo ndiyo yenye maamuzi ya mwisho, hivyo kero zao zitafika moja kwa moja kwa wahusika na baada ya mapendekezo hayo kutolewa maamuzi watajulishwa.

“Kero zote zitawafikia wahusika hasa Bunge ambacho ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanyia kazi maoni yenu, lakini pia katika wizara husika ambayo ndiyo yenye maamuzi ya mwisho na baada ya mapendekezo yenu kutolewa maamuzi mtajulishwa,’’ alisema Kahatano.

Aidha, alithibitisha kuwapo na malalamiko ya wadau wa sekta ya usafirishaji juu ya kutumika kwa mfumo wa ufatiliaji wa magari (VTS) unaosemekana kuwa siyo rafiki kwa wamiliki hao na kudai kuwa mfumo huo ni sehemu ya gari kama sehemu nyingine na kazi ya kifaa hicho ni kudhibiti mwendokasi.

“Mfumo wa VTS ni sehemu ya gari kama sehemu nyingine kazi yake ni kudhibiti mwendo wa gari na ndio maana madereva wengi hawakubaliani nao kwasababu wanavunja baadhi ya kanuni za usalama barabarani, ifike wakati tukubaliane kuwa sote tuna lengo moja hivyo tushirikiane katika kutoa huduma bora na salama kwa wananchi,’’ alisema Kahatano.

Aidha alieleza kwa kile kilichosemekana kuwa wanashirikiana na kituo cha Taifa cha Utunzaji wa kumbukumbu (NIDC) ili kutoa tozo kwa wamiliki wa mabasi na kusema kuwa wadau waliotafutwa na LATRA ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na siyo NIDC wao wamepewa maagizo na Waziri wa Uchukuzi.

Naye, Mtaalam wa mifumo ya kutunza kumbukumbu, Cathbeth Simalengo, alieleza baadhi ya faida za mfumo wa kielektroniki ambao utakua unatumika kukata tiketi kwa njia ya mtandao kuwa ni pamoja na kuongeza kipato kwa wamiliki, kuweza kukata tiketi kokote utakapokuwa.

Alisema pia itasaidia mmiliki kujua wakina nani wamepanda gari lake na pia mfumo huo utarahisisha ukusanyaji wa mapato.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mpaka sasa mfumo uko tayari kiufundi na mfumo wao utakua ni wa gharama nafuu kuliko mifumo mingine yote ambapo hela za watu watakao kata tiketi zitaingia moja kwa moja katika akaunti za wamiliki wa magari hayo na hivyo usajili wa wamiliki utaanza hivi karibuni.

Naye Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Mkada Mkada, aliishukuru Taboa kwa mkutano huo na kuwataka watekeleze yale yote yaliyojadiliwa kwa ushirikiano.

Habari Kubwa