SMZ yajivunia mafanikio SADC

19Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
SMZ yajivunia mafanikio SADC

SERIKALI ya Zanzibar  imejifunza mambo mengi yenye manufaa katika mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Nchi Wanachama wa Ushirikiano wa Maendeleo (SADC), uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Hassan Khamis Hafidh.

Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara na Viwanda, pamoja na mkutano huo, pia imenufaika na maadhimisho na maonyesho ya nne ya wiki ya viwanda ya nchi wanachama wa  SADC.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri Hassan Khamis Hafidh, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, wakati akijibu suali aliloulizwa na mwakilishi wa Jimbo la Mpendae Mohammed Said, aliyetaka kujua ni faida gani zilizopatikana katika kuhakikisha viwanda na bidhaa za Zanzibar zinapata masoko mapya katika nchi wanachama wa SADC.

Naibu Waziri, alisema miongoni mwa faida zilizopatikana  ni kuanzisha mahusiano ya kibiashara kati ya wazalishaji wa viwanda kutoka Zanzibar na wanachama wa SADC.

Alisema pia Zanzibar imepata masoko mapya ya bidhaa ambayo yatawezesha kuinua uchumi wa wafanyabiashara na taifa kwa ujumla.

Naibu Waziri alieleza kuwa pia wameweza kujifunza namna ya kuhifadhi bidhaa na umuhimu wa vifungashio katika kuuza bidhaa katika soko la kimataifa la ukanda wa Kusini mwa Afrika.

“Faida nyingine ni kupata fedha kutokana na mauzo ya bidhaa za wajasiriamali  katika wiki ya maadhimisho na maonyesho,” aliongeza.

Aidha, akijibu swali lingine la ziada lililoulizwa na mwakilishi huyo, aliyetaka kujua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejifunza nini katika mkutano huo mkubwa na wa kihistoria katika kuharakisha shughuli za maendeleo, Naibu Waziri Hafidh, alisema:

“Serikali imejifunza ushirikishwaji wa sekta binafsi katika masuala ya kimaendeleo, kuongeza nguvu katika sekta ya kilimo na kuziongezea thamani bidhaa kwa maendeleo ya kiuchumi na viwanda.”

Alisema pia wamepata fursa ya kuwapa nafasi maofisa wa serikali kushiriki kikamilifu kwenye shughuli hiyo ili kujua mwelekeo wa SADC na kuaandaa mikakati imara ya kibiashara na kimasoko pamoja na kuainisha miundombinu wezeshi kwa maendeleo ya viwanda nchini.

Habari Kubwa