Aagiza vikundi wenye ulemavu kupewa mkopo

19Sep 2019
Woinde Shizza
LONGIDO
Nipashe
Aagiza vikundi wenye ulemavu kupewa mkopo

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  Joseph Nyamuhanga, ameziagiza halmashauri zote nchini, ambazo bado hazijatekeleza sheria ya kutoa asilimia 10 ya mapoto ya ndani kwa wanawake, vijana na walemavu kutenga fedha hizo na kuzigawa kwenye makundi hayo, kuanzia

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),  Joseph Nyamuhanga.

Aliyasema hayo wakati alipotembelea kikundi cha watu wanaoishi na ulemavu cha Tumaini Ushiriki kilichopo wilayani Longido mkoani hapa.

Akiwa Tumaini alijionea mambo mbalimbali yanayofanywa na kikundi hicho ikiwamo unenepesha wa mbuzi kwa ajili ya kuwauza  kwa faida.

Nyamuhanga alisema kuwa serikali haitamfumbia macho mkurugenzi yeyote wa halmashauri ambaye atashindwa kutekeleza sheria hiyo ya kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo.

Aidha, alieleza kuwa njia pekee ya kuisaidia serikali ni kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kwa kuhahikisha wanapata mikopo hiyo, itakayowainua kiuchumi.

Aliipongeza halmashauri ya Longido kwa kutekeleza sheria hiyo kwani hadi sasa wameshaviwezesha vikundi hivyo, kwa kuwapatia kiasi cha Sh. milioni 50.

Pia alikisifu kikundi hicho, kwa kufanya kazi ya kunenepesha mbuzi kwa ajili ya kuwauza na alisema kazi hiyo itawaongezea kipato mara dufu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Katibu wa Chama cha Watu wenye Ulemavu wilayani Longido,  ambaye pia ni mwanachama wa kikundi hicho, Emanuel Taraiya, aliishukuru serikali kwa kuwajali, kuwawezesha na kuwaendeleza kwa kuwapa mkopo watu wenye ulemavu.

Aidha, aliiomba serikali kutenga bajeti kwa ajili ya kuwapa elimu watu wenye ulemavu ili  wasikae ndani badala yake  watoke nje na  wapaze sauti kutokana na walemavu wengi kutokuwa na elimu ya kutambua haki zao.

Katibu wa Kikundi  cha Tumaini, Kitoitoi Ole Ndwati, alisema kuwa kikundi chao kinafanya kazi ya kunenepesha mifugo kwa ajili ya kuiuza katika masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Alisema kikundi hicho, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kukosa masoko, mazingira magumu ya kufanyia kazi, kuwa na mitaji midogo na ushuru wa mifugo kupanda kwa kiasi kikubwa hali inayowafanya kukosa wateja wa kununua mifugo yao.

Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Longido, Grace Mgase, alisema awali walipoanza mpango wa ugawaji wa mikopo hiyo, makundi ya watu wanaoishi na  ulemavu yalikuwa yamesahaulika na iliwawia vigumu kupata mikopo hiyo.

Alisema baada ya changamoto hiyo kujitokeza mwanzo waliitatua mapema kwa kuwatafuta na kuwakusanya watu wenye ulemavu na vilipatikana jumla ya vikundi 11 na vyote vilipatiwa mkopo huo.

Habari Kubwa