Upatikanaji maji Rombo chini ya asilimia 50

19Sep 2019
Godfrey Mushi
ROMBO
Nipashe
Upatikanaji maji Rombo chini ya asilimia 50

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitilya Mkumbo, amekiri kuwapo kwa hali mbaya ya upatikanaji wa huduma za maji katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro ambayo ni chini ya asilimia 50.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitilya Mkumbo

Katika kukabiliana na tatizo hilo, tayari wizara hiyo imetangaza mpango wake wa kutumia kiasi cha Sh. bilioni 10, ili kunusuru hali hiyo isiendelee kuwaumiza wananchi katika vijiji 40 vyenye hali mbaya zaidi.

Profesa Mkumbo, alikuwa akizungumza jana katika mahojiano maalumu na kituo kimoja cha redio katika Manispaa ya Moshi.

"Bahati mbaya Rombo, kwa Mkoa wa Kilimanjaro ndiyo ambayo ina hali mbaya sana ya upatikanaji wa maji ambayo ni chini ya asilimia 50, ukilinganisha na Siha yenye asilimia 80 na Hai asilimia 80.

"Wizara ya Maji imeliona hili na serikali inakwenda kutekeleza mradi mkubwa sana wa maji ambao utapeleka kwenye vijiji 40 vya Rombo na tunawakabidhi mradi huo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) watafanya hiyo kazi."

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo kwa kuanzia mwaka huu, wizara hiyo imetenga Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuanza utekelezaji na katikati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu, serikali itakuwa imetangaza zabuni ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika Wilaya ya Rombo.

Hali hiyo inatajwa kutishia ukuaji wa kiuchumi wa vijiji vilivyopo katika Wilaya ya Rombo kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji kwa miongo kadhaa sasa.

Nyakati za kiangazi, Wilaya ya Rombo huathiriwa zaidi na uhaba wa maji kutokana na kupungua kwa ujazo kutoka mita za ujazo 27,000 hadi kufikia 18,000.

Taarifa zaidi za serikali, zinaonyesha kuwa mahitaji ya maji wilayani humo ni mita za ujazo zaidi ya 40,000, lakini upatikanaji wa maji ni mita za ujazo 27,000.