Mil. 7/- zatengwa kununua taulo za kike

19Sep 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Mil. 7/- zatengwa kununua taulo za kike

BAADHI ya wadau wanaotetea ustawi na maendeleo ya watoto wa kike wameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutenga Sh. milioni 7.5 katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 za ununuzi wa taulo za kike.

taulo za kike

Walisifu hatua hiyo kuwa itapunguza utoro na kuongeza ufaulu kwa wasichana.

Wakizungumza juzi wakati wa kikao cha uchambuzi wa bajeti kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia TGNP na kuwahusisha viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa pamoja na viongozi wa halmashauri walisema hatua hiyo ni muhimu katika kumwezesha mtoto wa kike kusoma kwa utulivu.

Mwenyekiti wa Vituo vya Taarifa Wilaya ya Mbeya, Flora Mlowezi, alisema uamuzi wa kuweka bajeti ya Sh. milioni 7.5 kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike ulichagizwa na ushawishi wa kutoka TGNP-Mtandao ambao ulitoa hoja mbalimbali zinazoeleza faida ya kuwanunulia watoto wa kike pedi.

Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imekuwa ya mfano nchini kutenga bajeti ya ununuzi wa pedi ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2017/2018 walitenga Sh. milioni moja, mwaka 2018/2019, Sh. milioni tano na sasa Sh. milioni 7.5

“Sisi vituo vya taarifa vya maarifa kama sehemu ya mtandao wa jinsia Tanzania tunajivunia kuwa sehemu ya kuwezesha watoto wa kike kusoma kwenye mazingira ya utulivu, tunaipongeza halmashauri kwa kutambua adha wanazozipata watoto wa kike na kuona haja ya kutenga bajeti kwa ajili ya kuwasaidia pedi,” alisema Mlowezi.

Ofisa Programu Mwandamizi wa Mtandao wa Jinsia, Zainab Mmari, alisema hatua hiyo ni muhimu kwa mtoto wa kike kwani itachagiza ufaulu wa masomo na kupunguza utoro ukilinganisha na hali ilivyo sasa.

Alisema katika tathmini zao miongoni mwa sababu zinazosababisha watoto wa kike kufanya vibaya kwenye masomo yao inatokana na suala la hedhi kwani kipindi hicho humfanya mtoto kushindwa kuzingatia masomo kutokana na hali hiyo na mbaya zaidi wengine hushindwa hata kumudu gharama za kununua pedi kwa sababu ya umaskini kwenye familia zao.

Mmari alisema TGNP- Mtandao wataendelea kufanya kazi kwa karibu na Wilaya ya Mbeya kwa sababu imeonyesha mwitikio kwa masuala mbalimbali yahusuyo jinsia ikiwamo sekta ya elimu, afya, kilimo na maji.

Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbeya ambaye ni Ofisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji, Gidion Mapunda, alisema katika mwaka wa fedha 2018/2019 shule 16 zikiwamo za msingi na sekondari ziligawiwa pedi.

Alifafanua kuwa jumla ya shule 4,720 za msingi na sekondari wanafunzi wake walinufaika na pedi hizo wakiwamo wanafunzi wa Sekondari za Iwiji, Imezu, Itala, Ilunga, Teule na msingi ni Mshewe, Chang’ombe na Nsongwi juu.

Habari Kubwa