Samatta aandika rekodi kali Ulaya

19Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Samatta aandika rekodi kali Ulaya
  • *** KRC Genk pia yaruhusu rekodi ya hat-trick ya Raul, Rooney kufikiwa wakati ikitobolewa mabao 6-2, lakini...

STRAIKA wa kimataifa wa Tanzania na nahodha wa Taifa ya Stars, Mbwana Samatta ameweka rekodi mbili kwa mpigo, kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza na kufunga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini akishuhudia pia timu yake ya KRC Genk ikichapwa mabao-

Mshambuliaji wa KRC Genk, Mtanzania Mbwana Samatta, katika harakati za kuwania kumiliki mpira dhidi ya beki Red Bull Salzburg, kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya makundi iliyopigwa Uwanja wa Red Bull Arena mjini Wals-Siezenheim, Austria na wenyeji kushinda 6-2.

-6-2 na wenyeji wao, Red Bull Salzburg ya Austria.

Kwa rekodi hiyo Samatta ambaye alirejea uwanjani baada ya kukosekana kwenye mchezo wa Ligi ya Ubelgiji Ijumaa iliyopita kufuatia kuumia akiichezea Taifa Stars, sasa amempiku Kassim Manara aliyekuwa akishikilia rekodi ya muda mrefu ya kuwa Mtanzania pekee aliyecheza michuano ya klabu barani Ulaya, iliyokuwa ikijulikana kama Kombe la Washindi akiwa na klabu ya SK Austria Klagenfurt, michuano ambayo sasa inajulikana kama Europa League.  

Katika mechi hiyo ya Kundi E, linalozijumuisha pia mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Liverpool ya England na Napoli ya Italia, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Red Bull Arena mjini Wals-Siezenheim, Samatta alifunga bao hilo dakika ya 52 kwa kichwa ikiwa ni baada ya lile la kwanza la Jhon Lucumi la dakika ya 40.

Mbali na rekodi hiyo ya Samatta, lakini pia mechi hiyo iliandika rekodi kibao ambapo kinda wa Salzburg, Erling Haaland alijitangaza mwenyewe kuwa mchezaji wa kwanza katika michuano hiyo hatua ya makundi msimu huu kuweza kutupia hat-trick.

Aidha, Salzburg imefunga mabao mengi katika dakika 45 za kwanza (mabao matano) kuliko ilivyofanya msimu wa 1994-95 (mabao manne katika mechi sita).

Kwa ujumla Genk (imecheza mechi 13, haijashinda na kupoteza sita), sasa imecheza mechi nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya bila kuibuka na ushindi kuliko timu yoyote ile kwenye historia ya michuano hiyo.

Hata hivyo, mabao nane yaliyofungwa katika mechi hiyo kati ya Salzburg na Genk kwa ujumla ndiyo idadi kubwa katika siku moja ya kwanza ya michuano hiyo, idadi nyingine ikiwa ni mechi kati ya Hamburg na Juventus msimu wa 2000-01 iliyomalizika kwa mabao 4-4 na Olympiacos dhidi ya Bayer Leverkusen msimu wa 2002-03 ikimalizika kwa mabao 6-2.

Haaland akiwa na umri wa miaka 19 na siku 58 - ni mchezaji wa tatu kinda zaidi kuweza kufunga hat-trick kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa nyuma ya Raul (miaka 18 na siku 113, akifanya hivyo mwaka 1995) na Wayne Rooney (miaka 18 na siku 340, mwaka 2004).

Samatta na Genk yake sasa wanasubiri kuwakaribisha wababe wa Liverpool, Napoli hapo Oktoba 2, mwaka huu wakati Salzburg ikitarajia kuwafuata mabingwa hao watetezi katika Uwanja wa Anfield siku hiyo.

Licha ya ushindi huo wa kishindo wa Salzburg, bado ina kazi ngumu kuhakikisha inafuzu hatua ya 16-bora na mtihani wa kwanza itapaswa kuuthibitisha itakapokutana na Liverpool ambayo imetoka kuchezea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Napoli.

Mabao mengi ya Salzburg  katika mechi hiyo yalifungwa na Hwang Hee-chan, Dominik Szoboszlai na Andreas Ulmer

Habari Kubwa