Jela miaka miwili kwa kufanyakazi bila kibali

19Sep 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jela miaka miwili kwa kufanyakazi bila kibali

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imemhukumu Meneja  wa Kampuni ya Fuel Security Co. Ltd., Malcom  Doherty, kulipa faini ya zaidi ya Sh. milioni 11 au kwenda jela miaka miwili-

-baada ya kukutwa na hatia ya kufanyakazi nchini bila kibali, kutoa taarifa za uongo na kujiingiza kwenye ajira bila kibali.

Mshtakiwa huyo raia wa Uingereza amehukumiwa juzi katika mahakama hiyo.

Hukumu hiyo, ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Alisema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo katika mashtaka yote matano yaliyokuwa yakimkabili.

Alisema mshtakiwa amekutwa na hatia kwa mashtaka yote na kwamba atalipa faini ya Sh. 500,000 kila kosa kwa makosa mawili au kwenda jela mwaka mmoja mmoja.

Pia, alidai kuwa mshtakiwa atalipa faini ya Sh. 100,000 au jela mwaka mmoja kwa makosa mawili.

"Mahakama yangu inakuhukumu kulipa faini ya Sh. milioni 10 au kwenda jela miaka miwili baada ya kukutwa na hatia ya kujiingiza katika ajira bila kibali," alisema Hakimu Simba wakati akitoa adhabu hiyo.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa aliingia nchini bila kibali, kuishi nchini bila kibali na kuwandanganya maofisa Uhamiaji kuhusu uraia wake. Kutokana na makosa hayo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini ya Sh. 500,000 kila kosa.

Mashtaka mengine ni kutoa taarifa za uongo kuwa yeye ni Mtanzania wakati akijua si kweli, kwa kosa alitakiwa kulipa faini ya Sh. 100,000 au jela mwaka mmoja.

Mshtakiwa huyo alishindwa kulipa fedha hizo na amepelekwa gerezani.

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo aliiomba mahakama msamaha kwa kuwa ni raia mwema, ana mke ambaye ni Mtanzania na kwamba aliibiwa hati yake ya kusafiria.

Katika kesi hiyo, mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 19, 2017 katika Ofisi za Uhamiaji Wilaya ya Kigamboni , Dar es Salaam.

Habari Kubwa