Kabendera adai kukabiliwa tatizo la pingili za mgongo

19Sep 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kabendera adai kukabiliwa tatizo la pingili za mgongo

MWANDISHI wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera anayekabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi ikiwamo kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha wa zaidi ya Sh. milioni 100, ameiambia mahakama kuwa amepata matibabu na majibu ya awali yameonyesha ana matatizo ya pingili za mgongo.

MWANDISHI wa Habari za Uchunguzi, Erick Kabendera.

Pia, amedai kwamba amepata vipimo vya damu majibu yake anatarajia kupata mwisho wa wiki.

Madai hayo aliyatoa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile wakati akimpa taarifa kuhusu kupata huduma za matibabu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi Jebra Kambole alidai kuwa amesikia hoja ya serikali, lakini anaiomba mahakama kumsikiliza mshtakiwa kuhusu taarifa ya matibabu yake.

Hakimu alimhoji mshtakiwa kuhusu malalamiko yake ya matibabu kama yamefanyiwa kazi au la.

Mshtakiwa alidai kuwa juzi alipelekwa Hospitali ya Amana na kufanyiwa vipimo mbalimbali ikiwamo kupigwa X-ray na damu.

"Mheshimiwa majibu ya awali yameonyesha nina matatizo ya pingili za mgongo na majibu ya damu natarajiwa kupata mwishoni mwa wiki," alidai Kabendera.

Alidai kuwa kwa sasa ameshapata huduma ya vipimo anasubiri matibabu na kwamba hana malalamiko mengine.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa tena Oktoba Mosi, mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Katika kesi ya msingi, Kabendera anadaiwa katika siku tofauti kati ya Januari 2015 na Julai 2019 katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, alitoa msaada katika genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia faida.

Pia anadaiwa bila kuwa na sababu za msingi kisheria alishindwa kulipa kodi ya Sh. 173,247,047.02 ambayo ilitakiwa ilipwe kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)

Shtaka la tatu anadaiwa alijipatia Sh. milioni 173.2 wakati akijua kuwa fedha hizo ni za kutakatisha na zao la makosa tangulizi ya kukwepa kodi na kujihusisha na genge la uhalifu.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Habari Kubwa