Wahukumiwa kunyongwa kuua kwa kukusudia

19Sep 2019
Ibrahim Yassin
SONGWE
Nipashe
Wahukumiwa kunyongwa kuua kwa kukusudia

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, imewahukumu kunyongwa hadi kufa vijana watatu baada ya kukutwa na hatia ya kuua kwa kukusudia.

Waliohukumiwa ni Nathaniel Elias (31), Moses Kasitu (26) na Elias Mzumbwe.

Akitoa hukumu hiyo Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Dk. Adam Mambi, alisema mahakama imetoa hukumu hiyo kutokana na kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka ili adhabu hiyo iwe fundisho kwa wengine ambao wanapenda kujipatia mafanikio kwa njia za mkato kwa kusababisha mauaji.

Awali, akisoma shauri hilo Jaji Mambi, alisema washtakiwa hao walitenda kosa hilo Julai 25, 2014 eneo la Mpemba katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma Wilaya ya Momba, mkoani Songwe.

Jaji Mambi aliongeza kuwa washtakiwa walimvamia na kumuua Vascal Njowela, akiwa ametoka dukani alikokuwa akifanya biashara na alikuwa akielekea kwa bosi wake kupeleka mauzo ndipo alipokutana na wauaji hao akiwa getini kwa bosi wake huyo na kumuua kwa kumpiga risasi, na kuchukua kiasi cha Sh. milioni moja.

Wakili wa utetezi Jastian Mshokolwe, adai kuwa kulingana na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa mashtaka hana budi kukubaliana na hukumu hiyo huku akisema nafasi ya rufani kwa wateja wake bado ipo.

''Sinabudi kukubaliana na hukumu hiyo, lakini nafasi ya kukata rufaa kwa wateja wangu bado ipo, haki itaendelea kutafutwa katika ngazi za juu,'' alisema Mshokolwe.

Naye Wakili wa Serikali, Shindani Michael, kwa upande wake ameishukuru mahakama kwa kutenda haki kwa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa wananchi wengine wenye nia ya kufanya makosa kama hayo.

Nje ya mahakama, wananchi kwa upande wao, wakiongozwa na Adam Juma, waliipongeza mahakama hiyo kwa hukumu hiyo, wakisema kuwa vitendo vya ukatili katika mkoa huo vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara na kwamba kwa adhabu hiyo anaamini wataogopa kutenda mauaji.

''Ni ukatili mkubwa uliofanyika kuua na kupora fedha tena milioni moja, huu ni unyama usio na kifani, tumechoka kusikia mauaji yakiendelea mkoani kwetu, maana kila kukicha utasikia auawa kwa wivu wa mapenzi, mara dereva bodaboda auawa na kuporwa pikipiki, hii ni aibu,'' alisema Juma.

Habari Kubwa