45 mbaroni kwa kuuza petroli kwenye makazi

19Sep 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
45 mbaroni kwa kuuza petroli kwenye makazi

WATU 45 wamekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kosa la kufanya biashara ya kuuza mafuta ya petroli na dizeli katika makazi yao bila leseni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto.

Watu hao wamekamatwa katika operesheni iliyoendeshwa na jeshi hilo na pia kukamata lita 2,118 za petroli na dizeli lita 2,327 zilizokuwa zikiuzwa katika makazi ya watu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu operesheni hiyo jijini hapa jana, alisema imefanyika chini ya Wakuu wa Polisi wa Wilaya zote (OCD) za mkoa huo.

Alisema lengo la operesheni hiyo ni kukomesha biashara ya mafuta hayo ambayo hivi sasa imekuwa ikishamiri katika makazi ya watu kinyume na sheria.

Alisema biashara hiyo ni hatari kuendelea kufanywa katika makazi ya watu kwa kuwa inahatarisha maisha kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kulipuka kutoka na aina ya mazingira inavyohifadhiwa.

"Lazima wananchi wajifunze kutokana na tukio lililotokea kule kwa wenzetu wa Mkoa wa Morogoro, lori la mafuta liliporipuka na kuuwa vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya taifa na kulitia hasara taifa ya kuwatibia majeruhi," alisema Kamanda Muroto.

Pia Kamanda Muroto aliwataka watuhumiwa hao 45 waliokamatwa kuacha kuendelea kujihusisha na biashara hiyo kinyume cha sheria.

"Nitowe wito kwa wanachi, vijana hawa tulio wakamata wengi wao umri ni kuanzia miaka 18 hasi 38 umri ambao ni nguvu hivyo basi waachane na tabia hiyo na kufanya shughuli nyingine itakayo waingizia kipato," alisema.

Katika operesheni hiyo wilayani Mpwapawa, jeshi hilo lilikamata watuhumiwa saba, Chemba watuhumiwa watano, Bahi (1), Kongwa (8), Chamwino (13), Kondoa (2) na Dodoma jiji (7).

Katika tukio jingine Kamanda Muroto alisema wamekamata noti bandia zenye thamani ya Sh. 1,920,000 katika kijiji cha Chinugulu wilayani Chamwino mkoani Dodoma kwenye mnada.

Vilevile jeshi hilo linamshikilia Happy Gidioni (42), mkazi wa Kizota jijini Dodoma akiwa na pombe haramu ya moshi (gongo) lita nane na misokoto 20 ya bangi na bangi kavu isiyosokotwa nusu kilo.

Habari Kubwa