Tume yataka askari wapige kura siku 1 kabla uchaguzi

19Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tume yataka askari wapige kura siku 1 kabla uchaguzi

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesema inatarajia katika Uchaguzi Mkuu ujao, watendaji wake na askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wapige kura siku moja kabla ya uchaguzi wenyewe.

Imesema lengo ni kuyapa makundi hayo haki ya kupiga kura na kutekeleza majukumu yake ipasavyo siku inayofuata ya uchaguzi.

Hata hivyo, suala hilo limepingwa vikali na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, wakidai kuonyesha hofu ya utaratibu huo kutumika kuchakachua matokeo halali ya kura za wananchi.

Mkurugenzi wa (ZEC), Thabit Idarous, alisema kura hiyo itawahusisha vikosi vya ulinzi na usalama na watendaji wa tume hiyo ili watumishi hao watekeleze majukumu yao siku ya uchaguzi.

Aliyasema hayo wakati akifunguwa mafunzo ya siku tatu kwa waandishi wa habari kuhusu kuandika habari za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Idarous alisema hatua hiyo ya kura ya mapema imetokana na marekebisho ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar Na. 4 ya Mwaka 2018 ambayo inatoa nafasi kwa makundi hayo.

Alisema marekebisho hayo yamekuja baada ya kubainika askari makundi hayo hayaitumii haki ya kidemokrasia kupiga kura na kuwachaguwa viongozi kutokana na kutingwa na majukumu ya kazi katika siku hiyo.

''Marekebisho hayo sasa yatawapa nafasi baadhi ya watendaji waliokabidhiwa majukumu muhimu, kupiga kura siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika," alisema.

Wakati ZEC ikieleza hayo, vyama vya upinzani vimepinga vikali utekelezaji wa sheria hiyo, vikionyesha wasiwasi wa kuwapo kwa udanganyifu kuhusu kura zitakazotokana na makundi hayo.

Wakizungumza jana na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa vyama vya ACT-Wazalendo, CUF na Chadema walidai sheria hiyo ilipitishwa kwa nia ya kupendelea upande mmoja na kwamba vyama vya upinzani havikushirikishwa.

MBOWE ANENA

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alidai changamoto kubwa ni uhuru wa tume za uchaguzi za pande zote mbili.

Mbowe alidai tume hizo (ZEC na NEC) zinatumiwa vibaya kusaidia na kubeba upande mmoja pasipo kuzingatia sheria na kulinda maslahi ya wadau wote.

Alidai ndani ya tume hizo wameajiriwa makada wa chama cha siasa na wakati mwingine vyombo vya dola vinatumiwa kupiga kura kwa maslahi ya upande mmoja.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alidai jambo hilo limekuwa likifanyika hasa upande wa Zanzibar kwa askari kutoka Tanzania Bara kupelekwa visiwani huko kwenda kulinda amani lakini baadaye kutumika tofauti.

"Kwa utekelezaji wa sheria ya kupiga kura siku moja kabla, maana yake ni kuhalalisha wapige kura za ziada kwa ajili ya kupata ushindi kwa chama tawala," Mbowe alidai.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo wa Hai, mambo hayo yanafanyika kwa mpango maalumu ili siku ya kupiga kura vyombo vya ulinzi na usalama viwe na kazi ya kuwadhibiti wapinzani washindwe kupata haki kisheria."Tunataka tume huru ya uchaguzi ili haya mambo yafikiwe kwa maridhiano, watu wanaingia kwenye uchaguzi mkiwa hakuna mwafaka wowote, si sawa," Mbowe alishauri.

ZITTO AFUNGUKA

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema tangu awali walishaweka wazi kuwa mabadiliko ya sheria hiyo yana changamoto kubwa na yanaweza kuleta mtafaruku mkubwa visiwani huko kwa kuwa Baraza la Wawakilishi na serikali haijaridhiwa na wote.

“Baraza la Wawakilishi ni la chama kimoja, uamuzi umefanywa na upande mmoja na hatua walizochukua za kufanya mabadiliko ya sheria ni wa maslahi ya chama kimoja.

“Mabadiliko haya hayana maana, yatazuia vyama kukagua uhalali wa kura, hayaambatani na daftari, tofauti la watu wa vikosi, hapatakuwa na mawakala wa vyama kwenye kambi za jeshi," alisema.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alisema kutokana na uzoefu wa uchaguzi wa Zanzibar, maridhiano ili uchaguzi ujao ufanyike kwa hali ya amani, ni muhimu yakahusisha CCM na vyama vya upinzani.“Baada ya uchaguzi uliopita kufutwa, CUF na vyama vingine havikuunga mkono, hadi sasa hakuna mazungumzo yoyote kuhakikisha matatizo hayatajirudia, na sasa wamekuja na jambo lingine linalokwenda kuweka tatizo kubwa zaidi," Zitto alitahadharisha.

Zitto alisema utaratibu wa baadhi ya makundi kupiga kura siku moja kabla unafanyika kwa baadhi ya nchi, lakini akasisitiza kuwa tatizo kubwa ni mazingira hatari ya siasa za Tanzania yatakayochagiza uchaguzi kuvurugwa na kuhatarisha amani.

“ACT-Wazalendo tunaona mazungumzo yatakayopelekea mashauriano ni muhimu ili tuwe na uwanja sawa wa uchaguzi, ili Wanzanzibar wapate mtu aliyechaguliwa na wananchi wenyewe.

“Ni muhimu kutaka kuwa na mazingira ya kuwezesha uchaguzi uwe huru na haki, uchaguzi wa Zanzibar umekuwa na vurugu na kumwaga damu.

"Hadi sasa, haki ya uchaguzi wa Zanzibar haijakuwapo, ni muhimu mazunguzo kuwapo. Hadi sasa, hatutambui serikali na Baraza la Wawakilishi, ni muhimu pande zote zikubaliane badala ya tume kujiamulia, naamini Wazanzibar hawatakubali haki yao kuporwa tena," Zitto alidai.

KAULI YA CUFMsemaji wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdul Kambaya, alidai uamuzi wa ZEC kutekeleza sheria hiyo ni mbaya kwa mustakabali na ustawi wa demokrasia siyo tu visiwani Zanzibar bali kwa Tanzania nzima.

“Vyombo vya usalama visijengewe utaratibu wa kuhusishwa moja kwa moja katika uamuzi wa mgombea gani awe kiongozi kwa nafasi yoyote katika uchaguzi, kufanya hivyo kutajenga chuki miongoni mwa wananchi," Kambaya alitahadharisha.

Habari Kubwa