Maajabu tiba ya Askofu Mkuu Ruaw’ichi  kutoka KCMC - MOI

19Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Maajabu tiba ya Askofu Mkuu Ruaw’ichi  kutoka KCMC - MOI
  • Yawekwa rekodi ya gharama na ujuzi
  • Prof. Kahamba: Mwaka twapokea 100
  • Asimulia kinachomsibu, chanzo chake
  • JPM afunguka yake, aiahidi MOI ‘kitita’

ITAKUMBUKWA kuwa Agosti 15 mwaka huu, Muhashamu Askofu Yuda Tadeus Ruwa’ichi alitangazwa rasmi kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Rais John Magufuli (wa kwanza kulia), alipomjulia hali Muhashamu Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Yuda Thadeus Ruwa'ichi aliyelala kitandani, katika chumba cha uangalizi maalum. Anayefuata, ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface na madaktari mabingwa wa MOI.

Hiyo ni baada ya Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, kutangaza kung’atuka madarakani mwaka huu, baada ya kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo duniani, Papa Francisko kuridhia ombi lake.

Zikiwa zimetimia siku 27 tangu aanze kutumikia nafasi hiyo ya juu katika Kanisa hilo lililoenea duniani kote, Muadhama Askofu mkuu Ruwa’ichi, alipatwa na maradhi yaliyomfanya alazwe katika Hospitali ya Rufani ya KCMC, mkoani Kilimanjaro.

Wakati akiwa katika hospitali hiyo anafanyiwa upasuaji wa kichwa kutibu tatizo lililomsumbua, kukatokea ulazima wa kitaalamu, kutokana na kukwama kiufundi, hali iliyolazimu ahamishiwe katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili(MOI), jijini Dar es Salaam.

Ufafanuzi kitaalamu

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI, Prof. Joseph Kahamba, anasema, awali KCMC walimfanyia upasuaji Muhashamu Askofu Mkuu Ruwa’ichi, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya.

Anasema, baada ya kufanyiwa vipimo husika, walibaini kuwapo tatizo lenye uhitaji wa huduma iliyopo MOI kwa ajili ya matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa Prof. Kahamba, Muhashamu Askofu Mkuu Ruwa’ichi, alisafirishwa kwa ndege usiku na alipofika MOI, walianza kumfanyia vipimo na kubaini tatizo hilo.

“Ilipofika saa 7:00 usiku tulimuingiza chumba cha upasuaji na ulifanyika hadi saa 10:00 alfajiri chini ya madaktari bingwa wa upasuaji watatu,” anaeleza Prof. Kahamba.

Inaelezwa ndege hiyo ilitolewa na Rais Dk. John Magufuli, kufanikisha safari hiyo na mgonjwa kufika MOI usiku wa kuamkia tarehe 10 mwezi huu.

Kwa mujibu wa Profesa Kahamba, iwapo ingetokea   hajapata ndege hiyo, angelazimika kukodi kutoka ama Afrika Kusini au Kenya kwa gharama ya Dola za Marekani 300,000 (Sh. milioni 690) kwa ajili ya usafiri na kama mgonjwa angelazimika kwenda kutibiwa nchini Afrika Kusini, angelipa gharama ya kulala kwa siku ni Dola za Marekani 1,000 (Sh.milioni mbili na laki tatu).

“Kama mgonjwa angekaa hospitali kwa siku 10 ina maana angelipa Dola za Marekani 10,000 (Sh. milioni 23 za kitanda) ambazo ni takriban Sh milioni 30, gharama ambazo ni kubwa bila kujumlisha matibabu,” anasema na kuingeza:

“Haya ni mafanikio makubwa ambayo MOI tunajivunia kutoa matibabu ambayo awali wagonjwa walikuwa wanayafuata nje ya nchi.”

Kinachomsibu, tiba

Prof. Kahamba anasema, ugonjwa uliompata Muhashamu Askofu Mkuu Ruwa’ichi, siyo kiharusi kama wengi walivyoufananisha, bali ni damu kuvimba kwenye ubongo, ambao kitaalam unaitwa ‘Chronic Subdural Haematoma’.

“Tunashukuru hali ya mgonjwa inaendelea vizuri tofauti na kabla hatujamfanyia upasuaji. Alifika hapa usiku wa kuamkia Septemba 10, akitoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro,” Prof. Kahamba anasema.

Namna wanavyomtibu

Prof. Kahamba anasema wameunda timu ya wataalamu saba wanaomfanyia uchunguzi wa kina katika kuhakikisha afya yake inarejea kama ilivyokuwa awali.

Anataja fani za wataalamu wanaomfanyia uchunguzi Askofu Mkuu ni madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya: Ubongo, Dawa za Usingizi na Magonjwa ya ndani.

Pia, kuna wataalamu wanne ni wa masuala ya; chakula na lishe, mazoezi tiba, uchunguzi na uuguzi.

 Prof. Kahamba anaendelea: “Wataalamu hawa saba wa uchunguzi watafanya kazi hiyo ili kuhakikisha afya ya Askofu inarejea katika hali yake ya kawaida na huwa tunafanya kwa wagonjwa wengine wanaopata tatizo kama hili,”

Chanzo nini?

Prof. Kahamba anasema, sababu za ugonjwa huo hazijulikani, lakini ni tatizo linalowatokea watu wengi mara nyingi, katika mazingira ya vyanzo kama kuumia kichwani, shinikizo kubwa la damu linaloweza kusababisha mishipa ya damu kupasuka.

Lingine analitaja kuwa, matumizi ya dawa zikiwamo za kupunguza maumivu ambazo zinasababisha damu kulainishwa na kuvimbia kichwani.

Prof. Kahamba, anasema mgonjwa asipopata matibabu ya haraka damu, hatari yake damu inaendelea kuvuja kichwani na ujazo wake unapoendelea kuzidi, unachangia mgandamizo kwenye ubongo na athari kuongezeka kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.

“Mgonjwa wa namna hii anapaswa kupata matibabu ya haraka iwezekanavyo na mtu akishagundua ugonjwa huu anapaswa kupata matibabu ya dharura,” anafafanua Prof. Kahamba.

Anataja dalili ya ugonjwa huo inalingana na upande ambao tatizo linakuwa kwa mtu kichwani. Anataja dalili za jumla ni; kuumwa kichwa, kizunguzungu, dalili za kutapika na kukosa nguvu mkono na mguu mmoja.

Kilichoko MOI

Prof. Kahamba anasema, ugonjwa huo wa ‘Chronic Subdural Haematoma’ gharama za upasuaji nchini ni Sh. milioni nne, lakini kwenda nje ya nchi zinagharimu takriban Sh. milioni 20, ambazo ni wastani usiopungua mara tano ya gharama za sasa.

Aidha, anasema MOI wastani wao wanawafanyia upasuaji wagonjwa wawili kila wiki na takribani 100 kwa mwaka katika mafanikio hali zao kirejea vizuri.

“Ugonjwa kama huu unatibika MOI bila shida na tunafanya upasuaji kwa wagonjwa wengi hadi 100 kwa mwaka na wagonjwa wote wanapona na gharama zetu zote hadi malazi ni ndogo zinafika Sh. milioni nne, kulinganisha na nje ya nchi ambazo zinafika hadi Sh. milioni 20 kwa kila kitu,” Prof. Kahamba.

JPM ‘awapa tano’

Saa chache baada ya Muhashamu Askofu Mkuu Ruwa’ichi kufanyiwa upasuaji tarehe 10 ya mwezi huu, Rais Dk. John Magufuli, alimtembelea na kuipa pongezi uongozi wa MOI kwa huduma alizozisifu kuwa ‘nzuri.’

Rais Dk. Magufuli anatamka:“Niliongea na Askofu Msaidizi wakati huo wameelezwa na hospitali ya KCMC kwamba ni lazima Askofu Ruwa'ichi apelekwe MOI, palikuwa hakuna usafiri wa kumleta lazima wachukue ndege ya ‘ambulance’ (ya kubeba wagonjwa) ya kumleta.

“Ndege lazima ukodi Afrika Kusini au Kenya, basi wakati wanahangaika, nikasema madaktari wajiandae nitatuma ndege, ndipo nikatuma ndege haraka haraka ikaenda ikamchukua."

Rais Dk. Magufuli, anaungana na kauli kutoka MOI kwamba aina na kiwango cha matibabu ya upasuaji mkubwa MOI inatoa hivi sasa, awali haikupatikani nchini.

Katika kauli na pongezi yake. Dk. Magufuli, anawaambia madaktari na wauguzi wa MOI, kwa anatambua kazi kubwa wanayofanya na amewahidi kutoa Sh. bilioni 1.5 kwa taasisi hiyo, kwa ajili ya kununua vipandikizi vya wagonjwa wanaopatiwa matibabu hapo.

Mkurugenzi MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicius Boniface, anamshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kutoa fedha hizo na kuhakikisha kuwa zitasaidia katika matibabu ya Watanzania wengine.

Anasema idadi ya viongozi wa serikali wakitanguliwa na Rais Dk. Magufuli walienda kumjulia hali juzi na Mwakilishi wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fancis, ambaye alienda jana.

Dk. Boniface anawataja wengine ni Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Marek Solczynski, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa na maaskofu wengine.

Aliahidi kuwashauri ndugu zake kutengeneza kitabu cha watu wanaoenda kumuona, ili waandike salamu zao za kumtakia afya njema na kumuombea, ili kupunguza idadi ya wanaoingia wodini.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MOI, anasema wakati huo alipokuwa katika Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU), anapaswa kupata muda mzuri wa kupumzika kwa ajili ya kuangalia afya yake na kwamba waliwazuia kumuona, wakihofia pia maambukizi ya magonjwa.

Prof. Kahamba katika rai yake anawataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu na kumuacha kiongozi huyo apumzike wakati akiendela kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa za MOI, tangu juzi alitolewa kutoka chumba cha uangalizi maalum ana sasa amelazwa katika wodi ya kawaida na anafanyiwa mazoezi ya mwili.

*Makala hii inatokana na taarifa rasmi za MOI za katika mkutano na waandishi wa habari na nyinginezo kuhusu afya ya kiongozi huyo mwandamizi  wa kidini.

Habari Kubwa