Daktari anayeanza mafunzo kazini anasimulia ‘kimbembe’ darasa  uzazi

19Sep 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
Daktari anayeanza mafunzo kazini anasimulia ‘kimbembe’ darasa  uzazi
  • Afunguka ‘bifu’ lake na ushirikina

JUMAMOSI iliyopita gazeti hili lilibeba makala hii sehemu ya kwanza, simulizi mwanamke kijana wa Kitanzania aliyekuwa mwanafunzi bora katika kozi ya udaktari tiba ya binadamu chuoni kwake. Endelea kumfuatilia, kuhusu dira yake katika taaluma  anayoianza.

Dk Irene Mageni, akiwa na Waziri wa Afya Cuba. Dk José Ángel Portal Miranda, kwenye mahafali aliyotunukiwa tuzo ya Mwanafunzi Bora Mgeni, katika chuo cha Latin American School of Medicine, nchini Cuba.

IRENE Mageni ni mhitimu wa masomo ya udaktari nchini Cuba, ambaye amefanikiwa kuwa miongoni mwa wachache waliotunukiwa tuzo hivyo kuweka historia nzuri.  Alikuwa mwanafunzi bora chuoni kwake.

Ukimuona ni mrembo hasa, katika tafsiri rasmi ya urembo, lakini ndani yake ana faida ya ziada kuwa ni daktari wa kutibu binadamu.

Ana mwezi mmoja tangu arejee nchini, akiwa kwenye mchakato wa kukamilisha taratibu za kutambulika nchini, kushiriki kwenye  mafunzo ya vitendo kwa mwaka mmoja.

Dk. Irene baada ya kutimiza ndoto yake, tayari kuna mambo kadhaa ambayo amekusudia kuhakikisha kuwa anashirikiana kikamilifu na watangulizi wake, katika kuisaidia jamii akiamini ataweza.

Anabainisha kuwa, imani ya kishirikina ni miongoni  mwa mambo yanayowatesa baadhi ya wanajamii,  kuumia kiafya na hata kisaikolojia.

Daktari huyo mwanamke kijana, anaamini wapo watu kadhaa wamepoteza maisha kwa magonjwa, ilhali wangewahi kwenda hospitali, wangepata matibabu sahihi na pengine yangewasaidia kuendelea kuishi.

Dk. Irene anaeleza kuwa amebaini kuwapo watu wanaochelewa kwenda hospitali kutibiwa kila wanapougua. Imani katika hilo ni kwamba, wanabweteka katika dhana kuwa wamelogwa.

Hivyo, wanaamua kuzunguka kwa waganga wa jadi, licha ya magonjwa wanayougua yana tiba hivyo wangewahi kwenda kufanyiwa vipimo sahihi ili watibiwe ipasavyo.

“Baada ya kumaliza masomo yangu nakusudia kuitatumia elimu niliyoipata vyema, ikiwamo kuelimisha baadhi ya wanajamii kuacha kuamini masuala ya ushirikina na badala yake watambua umuhimu wa kupata tiba sahihi,’ anasema daktari huyo.

Pia,  anafafanua kuwa, magonjwa mbalimbali ambayo yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina, anayataja kuwa ni kifafa, malaria na shinikizo la damu.

UJUZI WAKE?

Anaeleza imani yake kuwa ameiva katika fani ya utabibu, kutokana na mafunzo ya vitendo aliyopata, ambayo kwa upande wake alikuwa akiyafanya kwa moyo wa ushujaa ikiwamo upasuaji mjamzito.

“ Hata hivyo, siku niliposhuhudia mjamzito anajifungua kwa njia ya kawaida, nilikumbwa na hali ya ajabu tofauti na mengine. Nilijikuta nashikwa na woga hadi machozi yalinitoka,” anasema Dk. Irene.

Anaeleza kadri alivyokuwa anashiriki mafunzo hayo, ndivyo alijikuta anapata ujasiri, kiasi cha kufikia kushiriki kusaidia mjamzito kujifungua kwa njia ya kawaida, aliyoihofia awali. 

Daktari huyo anasema, haikuwa kazi rahisi kwake kutimiza ndoto yake, kwani kuna mambo alikutana nayo yaliyomtia woga, lakini hakukata tamaa kwa kuwa wazazi wake walijenga katika dhana ya kutovunjika moyo na kujitambua.

Matokeo hayo mazuri aliyoyapata katika Latin American School of Medicine, anabainisha anaamini yatakuwa  chachu itakayowavutia  wanafunzi wengine hasa wa kike kusoma kwa bidii,  nao watimize ndoto zao.

ALIKOTOKEA

Irene, elimu yake ya msingi ameipata katika shule ya Gangilonga mjini Iringa na  kisha akahamia katika Shule ya Msingi, Karakata, Dar es Salaam, kabla ya kurejeshwa tena mjini Iringa kwenye Shule ya Msingi Lugalo,  alikohitimu darasa la saba.

Baada ya hapo, alijiunga na Shule Sekondari ya St. Francis jijini  Mbeya, alikomaliza kidato cha nne na akajiunga na kidato cha tano na sita, katika shule ya Marian Girls iliyoko Bagamoyo, alikohitimu mwaka 2012 na akapata nafasi ya kwenda nchini Cuba kusomea udaktari wa binadamu.

Wahenga wanasema ‘usione vyaelea jua vimeundwa.’ Ndivyo ilivyo kwa Dk Irene, ambaye ni zao la kutimiza ndoto kutokana na ushirikiano mzuri aliopata kutoka kwa wazazi wake.

 Mama mzazi wa Irene, Dorothy Magese, anayejitambulisha ni mihtimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Rugambwa, iliyoko mjini Bukoba, anaeleza hisia yake ya furaha kuona mtoto wake ametimiza ndoto ya kuwa daktari na kuongeza idadi  ya madaktari wanawake.

 “Wazazi jukumu letu kuhakikisha tunawapa moyo watoto wetu kwa kuhakikisha tunawawezesha, tunawashauri ili kuwasaidia kufanikisha kupata elimu ili waweze kutimiza ndoto za kufanya kazi za wanazozipenda, kwa kuwa watakuwa wanafanya kazi hizo kwa bidii hivyo kutakuwa na mafanikio kwa nchi na jamii,” anasema

SERA YA AFYA

Juhudi mbalimbali zinafanywa na serikali, taasisi binafsi na wataalam wa afya  kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa kupata matibabu mapema, badala ya kujichelewesha kwa kukibilia wenda kuagua kwa waganga wa jadi ambao wengi wanatajwa kuwa ni wadanganyifu na wachumia tumbo.

Sera ya Afya ya Mwaka 2007, inaeleza kuwa elimu ya afya na uhamasishaji ni njia mojawapo katika utoaji wa huduma za afya.

“Njia hii inatumia utaalamu wa mawasiliano na kutayarisha na kuwasilisha ujumbe mbalimbali kwa mtu binafsi, familia na jamii kwa lengo la kubadilisha mienendo na tabia zinazochangia kuwapo au kutokuwapo kwa maradhi katika jamii,” inaeleza. 

Kwa mujibu wa sera hiyo, mbinu mbalimbali ikiwamo ya kutumia vyombo vya habari, mabango, vipeperushi, majarida, vitabu na wavuti hutumika kushawishi na kuwasilisha ujumbe huo.

Sera hiyo inaeleza kuwa katika utekelezaji wa elimu ya afya na uhamasishaji, serikali imefanikiwa kutoa elimu ya afya kwa wananchi pamoja na kuwahamasisha namna ya kuzuia magonjwa ya kuambukiza. Magonjwa mengi yamedhibitiwa, hasa yale yanayoweza kuzuilika kwa chanjo.

“Hata hivyo, elimu ya afya inayotolewa bado haijaleta mabadiliko makubwa ya tabia na mienendo inayotarajiwa katika jamii,” inaelezwa.

 Mambo kadhaa yanatajwa, ikiwamo  mazingira yaliyopo kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa hayatoshelezi kila mtu kuweza kukuza, kulinda na kuendeleza afya yake.

Kunaorodheshwa madhumuni makuu ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kumuwezesha kila mtu kulinda na kuendeleza afya yake kwa ufanisi.

Tamko linalotolewa kwenye sera hiyo, ni kwamba serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaimarisha utoaji elimu ya afya, ili kumhamasisha na kumuwezesha kila mtu kujenga tabia inayozingatia kanuni za afya na maisha bora.

Pia, inaelezwa serikali kwa kushirikiana na wadau, itaandaa sheria, miongozo na  mikakati itakayowezesha kila mtu kupata elimu, ili kulinda, kukuza na kuendeleza afya bora.

Habari Kubwa