Malinzi adai hakuwahi kuandika madai ya fedha

19Sep 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Malinzi adai hakuwahi kuandika madai ya fedha

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amedai mahakamani hakuwahi kuandika madai ya fedha alizolikopesha shirikisho hilo, lakini alilipwa kwa kuwa ilikuwa ni taratibu na namna ya uendeshaji wao.

RAIS wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Malinzi alitoa madai hayo jana wakati akihojiwa na upande wa Jamhuri kuhusu ushahidi wake kwamba alilipwa fedha alizoikopesha TFF kihalali.

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa ushahidi wa utetezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamaba na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai, alimhoji mshtakiwa huyo kuhusu fedha alizolipwa kama aliandika malalamiko kabla ya kufanyika malipo hayo.

Mshtakiwa alidai kuwa TFF ilikuwa ina utaratibu huo wa kumlipa na ilifahamu kwamba ameikopesha fedha hizo.

Alidai kuwa mbali na kuikopesha TFF, aliwahi kufadhili mbio za marathoni kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo kiongozi wa michezo alikuwa marehemu Joel Bendera na baadaye alishika nafasi hiyo William Ngeleja.

"Bunge lilifadhili mbio za marathoni miaka saba kuanzia mwaka 1997 mpaka 2004," alidai Malinzi.

Hata hivyo, alidai kuwa Spika wa wakati huo pamoja na Mwenyekiti wa Bunge hawakumbuki ila anayemkumbuka ni kiongozi wa timu hiyo  marehemu  Bendera na  Ngeleja.

Alidai kuwa nyaraka zote zinazohusu ufadhili wa michezo mbalimbali ikiwamo ngumi za kulipwa zitakuwapo ofisini kwake katika Kampuni ya Cargo Star's.

Hakimu Kasonde alisema kesi hiyo inaendelea leo kusikilizwa utetezi wa washtakiwa.

Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine ni aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga na Karani Flora Rauya.

Katika kesi hiyo mashahidi 15 wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi na tayari aliyekuwa Rais wa TFF, Malinzi ameanza kujitetea.

Katika kesi hiyo washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335.