Kifaa cha ukaguzi KIA hakifanyi kazi miaka 3

19Sep 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Kifaa cha ukaguzi KIA hakifanyi kazi miaka 3

IMEELEZWA kuwa kifaa maalum cha ukaguzi wa mizigo ya wageni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hakifanyi kazi kwa miaka mitatu sasa kutokana na kuharibika.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Hali hiyo inasababisha watalii na wageni kupoteza mizigo yao, huku baadhi ya watendaji wakidaiwa kutokuwa waaminifu wakati wa usomaji wa kamera inapopotea mizigo ya wageni hao.

Changamoto hiyo iliibuliwa jana katika kikao cha pamoja kati ya wadau wa utalii wanaotumia uwanja huo, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, alisema serikali ililazimika kuitisha kikao hicho baada ya kuibuka malalamiko ya wadau wa utalii wakati wa mapokezi ya faru tisa, kati ya 10 wenye vinasaba vya faru wanaopatikana Tanzania, waliorejeshwa nchini Septemba 10, wakitoka Afrika Kusini.

"Siku ile tulipopokea wale faru, tulipokea malalamiko kutoka kwa wadau wa utalii ambao walikuwa wakilalamikia upotevu wa mizigo na Visa zao katika mfumo mpya wa njia ya mtandao (e-Visa).

"Walisema hiyo kwao ni changamoto kubwa ambayo inakwamisha biashara ya utalii nchini kwani utalii unahitaji ufanisi na uaminifu," Kanyasu alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Emmanuel Mollel, alisema: "Asilimia 90 ya wageni wanaoingia nchini wakipitia KIA hueleza masikitiko yao ya kupotelewa na mizigo yao na kusimama muda mrefu wakisubiri kuhakikiwa Visa zao, wanatumia zaidi ya saa tatu."

Alisema kitendo hicho huwachukiza wageni kutokana na kuchoka na hivyo kulalamika na hawapendi jambo hilo kujitokeza kwa kuwa linaweza kuua soko la utalii nchini.

"Mheshimiwa Naibu Waziri, kuharibika kwa 'screen' (kiambaza) hiyo kwa miaka kadhaa sasa ni changamoto kubwa kwa wadau wa utalii na watalii wenyewe katika kujua ratiba za ndege na katika kupata taarifa mbalimbali," alisema.

Mdau mwingine wa utalii kutoka Kampuni ya Zara Tanzania Charity, Bernard Sihini, alisema kuharibika kwa kifaa hicho na ukosefu wa dawati la taarifa ni mtihani kwao katika kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali.

Akijibu hoja za wadau hao wa utalii, Mkurugenzi wa Kampuni ya Uendeshaji na Uendelezaji wa KIA (Kadco), Christopher Mukoma, alisema changamoto hizo wanazifanyia kazi.

"Hicho kifaa maalum kimechukua muda mrefu kuwekwa kutokana na Sheria ya Ununuzi ya Umma kufanyiwa mabadiliko, lakini kwa sasa tumeshamaliza taratibu zote na siku yoyote kuanzia sasa kifaa hicho kitawekwa katika uwanja huo," alisema.

Sheria hiyo ya mwaka 2011 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alikiri kuwapo kwa upungufu katika sekta ya utalii na kikiomba kikao hicho  kuunda kamati ndogo itakayoshughulikia mambo mbalimbali yanayoikabili sekta ya utalii na viwanja wa ndege vya KIA na Arusha.

"Kutokana na  changamoto za utalii kuelezwa hapa, nakiomba kikao hiki kikubali uundwaji wa kamati  ya watendaji wa viwanja vya ndege, kampuni binafsi za utalii  na watendaji wa serikali wakiwamo maofisa Idara ya Uhamiaji ili ni kuona namna ya kuboresha utalii nchini," Gambo alishauri.

Mkuu wa mkoa huyo pia aliwataka wadau wa utalii kuacha chuki za kibiashara na kupendana wao kwa wao ili kuleta mabadiliko ya sekta ya utalii.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolph Mkenda, alisema kikao hicho kililenga kushughulikia usalama na ufanisi wa biashara ya utali nchini.

Habari Kubwa