Matatizo ya umeme Arusha mwisho 2025

20Sep 2019
Woinde Shizza
ARUSHA
Nipashe
Matatizo ya umeme Arusha mwisho 2025

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme (Tanesco), limewahakikishia wateja wake kuwa limejipanga kutatua na kumaliza tatizo la kukatikatika kwa umeme mara kwa mara mkoani Arusha litakuwa limemalizika kabla ya mwaka 2025.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Raymond Seya.

Hayo, yalisemwa na Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Mkoa wa Arusha, Raymond Seya, wakati akizungumza na waandishi wa habari, alipokuwa akifunga semina ya kuwajengea uwezo wahandisi wa matengenezo na mameneja wa shirika hilo wa mikoa na kanda ya kaskazini.

Alisema awali kulikuwa na tatizo la kukatika umeme mara kwa mara, lakini sasa hivi wamejipanga kutatua tatizo hilo, kwa kufanya maboresho zaidi kwenye sehemu mbalimbali ili usikatike mara kwa mara.

Aidha, alisema shirika hilo, litaendelea kuboresha utoaji wa huduma hiyo kufikia viwango vya kimataifa ili wateja waridhike na huduma wanayoitoa na wanayoipata.

“Lengo la semina hii ni kuhakikisha wahandisi wetu wanafanya kazi usiku na mchana kuwahudumia wateja ili  kwamba watatue tatizo la kukatikatika  kwa umeme ambayo ni kero inayolalamikiwa mara kwa mara kitendo kinachoisababishia serikali na shirika  ukosefu wa mapato,” alisema Seya.

“Mapato haya yanapotea  viwandani wakati umeme unapokatika, mfano kwenye kiwanda cha kutengeneza plastiki umeme ukikatika wakati wanaendelea kuzalisha kinachotokea ni kuharibu mtiririko waliokuwa wakitumia kutengeneza bidhaa hizo,” aliongeza Seya.

Alieleza kuwa ni matarajio yao kuwa watahakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma ya umeme ambao utakuwa wa uhakika kila siku na kila wakati.

Hata hivyo, alisema kuwa sera ya serikali ni kufikia uchumi wa kati na wa viwanda hivyo ni lazima waboreshe huduma ya umeme kuwa ya uhakika ili kuwavutia wawekezaji wengi.

Meneja Mwandamizi na Usambazaji wa Tanesco, Mhandisi Mahende Mgaya, alisema mafunzo hayo yalianza kwa kufuatilia na kuangalia chanzo kikuu cha kukatika umeme, kuanzia mwaka 2015 na baada ya hapo wakatengeneza mpango mkakati wa kutatua changamoto hiyo.

“Lengo letu ni kuweka mpango mkakati utakaoendana na sera ya nchi ili tuweze kufikia uchumi wa kati na viwanda ni lazima kwanza tuhakikishe tuna umeme wa uhakika na wakutosha na usio katikakatika mara kwa mara,” alisema.

Aliongeza kuwa lengo ni kuboresha mipango ya Tanesco ili  kupata na kuwavutia wawekezaji wengi kuwekeza viwanda hapa nchini," alisema Mgaya.

Aliongeza kuwa  kama nchi nyingine za  Afrika zimeweza kumaliza tatizo la kukatika umeme kwenye mataifa yao, basi hata Tanzania  linaweza kutatulika kama walivyofanya nchi kama Misri

Habari Kubwa