Mufti awapa neno Waislamu nchini

20Sep 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Mufti awapa neno Waislamu nchini

MUFTI wa Tanzania Sheikh Abuubakari Zuberi, amewataka Waislamu kujenga ushirikiano na kusaidiana ili kulijenga taifa na mshikamano ambao utaepusha migogoro kwenye jamii.

Mufti wa Tanzania Sheikh Abuubakari Zuberi.

Mutfi Zuberi aliyasema hayo, wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani hapa na kuwataka Waislamu kuendelea kuidumisha amani ya nchi, kwa lengo la kuondoa migogoro baina yao.

Alisema kuishi kwa vifundo sio maagizo ya Uislamu na aliwataka wale wenye vifundo vyao waache na kurudi kwa Mwenyezi Mungu kwani hakuna anayeijua kesho yake hivyo, ni bora kuwa na busara kwa kuwa mcha Mungu na kuishi kwa kuvumiliana na subira ndiyo mwongozo.

“Sio busara kuwa na migogoro ambayo imekuwa ikirudisha shughuli zetu za maendeleo nyuma wala tusiwe watu wa kulalamika kila mara tuchape kazi kwa kujiletea maendeleo na kufanya ibada, hilo ndiyo lengo la Uislamu na hiyo ndiyo Jihad,” alisema Mufti Zuberi.

Kwa mujibu wa Mufti huyo, aliwaomba Waislamu wote nchi kuishi kwa kupendana na kuheshimiana na kuwatendea wema wenzao ili kuwavuta kwenye dini.

Aidha, aliwaomba kuondokana na mitazamo yenye chuki baina yao na kuijenga jamii yenye ustaarabu kwani Uislamu unajengwa na mambo mawili makubwa kujitoa na kujitolea katika dini na maisha yao.

"Sasa naomba muishi kwa kufuata misingi ya dini kwa kuwa tuna Qura’an turudi huko pindi tunapohitilafiana," aliongeza Mufti.

Alisema amani ndiyo nguzo ya kuabudu kwa misingi ya kuijenga amani nchini, kwani bila amani ibada yenye utulivu haitakuwapo.

"Kwa kuwa Uislamu ulifika hadi Hispania, lakini walipopishana waliharibu kila kitu hadi bahari ikawa nyekundu, kutokana na wino wa vitabu hivyo, busara ndiyo iwe nguzo ya kuondoa changamoto na kuhakikisha amani inakuwapo," alisisitiza Mufti.

Habari Kubwa