Kiama chaja waliovamia shamba

20Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Kiama chaja waliovamia shamba

SERIKALI imesema itawaondoa kwa nguvu wananchi 48 waliojenga makazi ya kudumu katika Shamba la Fofo/Foo Estates, Hai, mkoani Kilimanjaro, ifikapo Septemba 23, mwaka huu, baada ya kukaidi amri ya kuhama eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya

Shamba hilo lenye ekari 46.6 lilifutwa hati yake na Rais na kutolewa kwa wananchi wa vijiji vya Urori, Mulama, Usari na Tella, vilivyoko Narumu, Tarafa ya Lyamungo.

Jana, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, alisema: "Niliwapa siku saba hao wananchi wawe wamevunja nyumba hizo wenyewe na kuondoka lakini wamekaidi.

“Waziri wa Ardhi (Nyumba na Maendeleo ya Makazi), William Lukuvi, alishatoa maelekezo na hatuwezi kuacha kusimamia maelekezo ya serikali. Jumatatu ijayo (Septemba 23) nitakwenda kutekeleza operesheni ya kuwaondoa."

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya, wananchi hao walijimilikisha shamba hilo wakiwa hawana haki ya umiliki kisheria. Shamba hilo lilifutiwa hati na Rais baada ya kubatilisha miliki Novemba 22, 1993.

Inaelezwa kuwa baada ya watu hao 48 kudaiwa kuvamia shamba hilo, mgogoro mkubwa wa umiliki wake ulizuka kati yao na wananchi wa vijiji vya Urori, Mulama, Usari na Tella ambao ni wanachama wa Chama cha Ushirika cha Narumu/Manushi.

Wiki iliyopita, wakati anazungumza na wananchi wa vijiji hivyo pamoja na waathirika hao 48, Ole Sabaya aliagiza kama kuna ujenzi wowote umeendelezwa usihamishwe na wananchi hao wabomoe nyumba zao.

“Nendeni kabomoeni nyumba zenu wenyewe ndani ya siku saba. Nawaapia kama Mungu aishivyo, nitakuja kusimamia ubomoaji wa nyumba hizo kwenye mashamba ya wananchi na kama mnadhani natania, nisubirini baada ya siku saba,” alisema.

"Kama kuna mazao ya msimu nataka yaondoke na si vinginevyo. Kwa mujibu wa sheria hayo ndio mazao tunayoyatambua. Kama kuna nyumba mkabomoe, mali ya wananchi irudi mikononi mwa wananchi na hayo yalikuwa ndiyo maelekezo ya Mheshimiwa Waziri (Lukuvi) aliyekuja hapa kusimamia haki hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Magufuli," alisisitiza.

Kumbukumbu zilizopo kwenye majalada zinaonyesha kwamba shamba hilo lenye mgogoro kati ya watu 48 na wanakijiji wa vijiji vinne, linatambulika kama Shamba la Fofo/Foo lenye namba 240 & 242 lenye hati namba NP 405 EP LOT 661 likiwa na ukubwa wa ekari 46.6

Kabla ya kuzuka kwa mgogoro huo, mmiliki wa awali, Dk. Athony Phones, alikopa Sh. 120,000 katika benki iliyojulikana The Land Bank of Tanganyika au National Development Credit Agency, Oktoba 18, 1961 na kuweka rehani shamba hilo.

Hata hivyo, inaelezwa kwamba Dk. Phones aliondoka nchini akiwa anadaiwa deni hilo na hivyo shamba hilo kuuzwa na benki kufidia mkopo huo.

Mwaka 1977, Chama cha Ushirika cha Narumu (kilichoundwa na vijiji vya Urori, Mulama, Usari na Tella) kilishinda zabuni hiyo na kutakiwa kulipa deni hilo.

Aidha, taarifa iliyotolewa katika mkutano wa hadhara na Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Hai, Jacob Muhumba, inaeleza kuwa chanzo cha mgogoro huo ni madai ya watu 48 kutaka kukabidhiwa Shamba la Fofo na benki, jambo ambalo lilipingwa na wanachama wa Chama cha Ushirika Narumu/Manushi.

Habari Kubwa