Mauzo ya kahawa yaingiza mabilioni

20Sep 2019
MOSHI
Nipashe
Mauzo ya kahawa yaingiza mabilioni

BODI ya Kahawa Tanzania (TCB) imeuza tani 68,000 za zao hilo na kuingiza pato la taifa Dola 123,185,587 za Kimarekani kwa mwaka 2018/2019.

kahawa.

Gunia moja la kahawa yenye uzito wa kilo 50 limeuzwa kwa dola 110 kwa kahawa yenye ubora wa hali ya juu na msimu 2019/2020 TCB imeuza tani 20,000 za kahawa bora katika mnada wa ndani na soko la nje moja kwa moja.

Mkurugenzi wa Ubora na Uhamasishaji Kahawa wa TCB, Frank Nyarusi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusu maandalizi Siku ya Kahawa Duniani inayofanyika Oktoba Mosi kila mwaka. Alisema msimu huu wanatarajia kukusanya tani 50,000.

Alisema unywaji wa kahawa  nchini umefikia asimilia nane kutoka asilimia nne na asilimia 92 inakwenda nje ya nchi na kwamba jitihada za makusudi zinahitajika kukuza matumizi ya unywaji wa kahawa hapa nchini ili kuimarisha soko la kahawa.

Alitaja faida za unywaji wa kahawa kuwa ni pamoja na kuimarisha afya, kiburudisho, kuchangamsha, kufikiri kwa haraka na kufanya uamuzi sahihi na kusaidia kuimarisha kumbukumbu.

Mkurugenzi huyo alitaja sababu nyingine ni pamoja na kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya gauti na tezi dume, kushambuliwa kwa figo, msongo wa mawazo, kansa ya ini na utumbo mpana.

Kwa mujibu wa Nyarusi, bei ya soko la kahawa msimu uliopita haikuwa zuri kwa wakulima kutokana na nchi mbali mbali ulimwenguni ikiwamo Vietnam kulima kahawa nyingi na hivyo kufurika katika soko la dunia.

Nyarusi alisema bodi imepata masoko mapya ya zao hilo India, China, Korea, Algeria, Afrika Kusini na nchi mbalimbali za Afrika yakiwamo mataifa ya kiarabu.

Alitoa wito kwa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) na Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) kubuni na kutengeneza mashine ya kuandaa kinywaji cha kahawa papo hapo (instant Coffee) kwa matumizi ya nyumbani, hoteli na  migahawa.

Alisema kutokana na jitihada za Rais  John Magufuli katika kuimarisha zao la kahawa nchini, kumekuwapo na ongezeko la viwanda vya kuongeza thamani ya zao la kahawa.

Nyarusi alisema viwanda vimeongezeka kutoka 18 hadi 31 mwaka huu, vikiwamo viwanda viwili vikubwa vinavyotengeneza kahawa iliyo tayari kwa wanywaji.

Alisema viwanda vya kukobowa kahawa na kuongeza thamani ya zao la kahawa vimeongezeka hadi kufikia 26, wakati viwanda vya kuchakata kahawa kuanzia shambani vikiwa vimefikia 487.

Habari Kubwa