Agizo halmashauri kutenga maeneo ya vijana

20Sep 2019
Idda Mushi
DODOMA
Nipashe
Agizo halmashauri kutenga maeneo ya vijana

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, ameziagiza halmashauri zote za wilaya nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwawezesha vijana kutekeleza miradi mbalimbali.

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde.

Miradi hiyo ni inayohusu kilimo, mifugo na uvuvi, na hatimaye kuwa na uwezo wa kujiajiri na kujikwamua na umaskini.

Mavunde alisema hayo baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo ya vijana kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi katika vijiji vya Dareda wilayani Babati mkoani Manyara na Hurui wilayani Kondoa mkoani Dodoma, inayotekelezwa na mradi wa uwezeshaji vijana Oye, unaotekelezwa na SNV kupitia Shirika la Maendeleo la SDC.

 

Akibainisha serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Waziri Mkuu, wamekuja na mpango mkakati mahususi wa kuwahusisha vijana kwenye kilimo kwa kutoa mafunzo na kubadilisha mitizamo yao kwa kuwa asilimia kubwa ya vijana wanaamini kilimo sio suluhisho ya matatizo yao na wanaamini katika kazi nyingine.

 

“Hatua ya kwanza ni kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwamo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Morogoro, kwanza kubadili mtizamo wa vijana na kuwafanya wakipende kilimo, lakini hatua ya pili tunafanya uwekezaji mkubwa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu na tumeanza na mpango mkakati wa kuwajengea uwezo vijana 100 nchi nzima,” alisema na kuongeza:

 

 “Kati yao, 80 watafundishwa kilimo cha mboga kupitia Green House yaani kitalu nyumba, ambazo tayari zimeshafungwa katika baadhi ya maeneo katika mikoa 12 na vijana 20 watajifunza kutengeneza kitalu nyumba, ili iwe ni sehemu ya ajira na tusipate gharama kubwa kuagiza toka nje ya nchi.”

 

Alisema hatua ya tatu wanayofanya ni kuwawezesha vijana kupitia mifuko ya maendeleo ya vijana na asilimia 10 za mapato ya halmashauri nchi nzima, hivyo alihimiza utengwaji wa maeneo hayo kusaidia miradi hiyo inayoanzishwa na vijana.

 

Alizitaka taasisi nyingine  nchini kushirikiana na serikali kutatua changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo, na kwamba kwa kushirikiana pamoja wataweza kuleta mapinduzi makubwa na falsafa ya uchumi wa viwanda itafanyika kivitendo.

 

Mshauri wa biashara wa mradi wa Oye, Faustine Msangila, alisema wameweza kusaidia vijana zaidi ya 8,000 kati ya 6,500 waliolengwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo iliyoanza mwaka 2016, katika mikoa ya Shinyanga, Manyara, Singida, Tabora, Dodoma, Morogoro na kwamba wana mpango wa kuendeleza awamu ya pili ya mradi huo ili kwa kushirikiana na serikali wawafikie vijana zaidi ya 20,000 katika mikoa mingi zaidi inayokadiriwa kuwa kati ya 10 hadi 15.

 

Mshauri wa ufuatiliaji na tathmini kutoka SNV, Rashid Byarushengo, alisema wamekuwa wakiwakusanya vijana na kuwapa mafunzo na zana mbalimbali za kilimo ikiwamo pampu za maji za kutumia mafuta, mipira ya mita inayokadiriwa kufikia 200 kwa kila kikundi, mbolea, viuatilifu, na kuanza kwa kuanzisha mashamba darasa ambayo huyatumia kama sehemu ya kujifunzia.

Habari Kubwa