Sera ya misitu yaiva, wadau wapendekeza

20Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sera ya misitu yaiva, wadau wapendekeza

WIZARA ya Maliasili na Utalii, imesema sera ya misitu imekamilika, lakini baadhi ya wadau hususan sekta binafsi wameomba wakae ili waipitie.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda.

Hayo aliyasema  jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Sera hii imekamilika lakini wadau wa sekta binafsi waliomba tukae tena chini wajaribu kuiangalia na kuipitia tulikuwa na mazungumzo mazuri,” alisema.

Alisema wadau walisema wafanye hivyo kama sehemu ya kuchangia uchumi wa viwanda na kuiangalia misitu kama fursa ya utalii.

“Tumekubaliana tutakuwa na mkakati ambao utachochea viwanda ambavyo vinatumia kwa ufanisi zaidi malighafi zitokanazo na misitu. Tunakaribia kukamilisha sera hii na kuiingiza kwenye mchakato ili iweze kukubalika serikalini,” alisema.

Prof. Mkenda alisema sera hiyo italeta mageuzi na kwamba misitu itakuwa siyo suala la uhifadhi bali kwa ajili ya viwanda na utalii.

Kuhusu nyuki, alisema: “Zamani tulikuwa na kiwanda kimoja Kibaha cha kuchakata asali sasa kimekufa, kingine kilikuwapo Kipalapala nacho kimekufa.”

“Sasa tumetenga takribani Sh. bilioni 1.8 kuanzisha viwanda vya kuchakata asali, tumekubaliana kabla ya kuanza kuwekeza kwa namna yoyote ile lazima tujue ni kwa nini vile viwanda vilivyokuwapo vimekufa,” alisema.

Alisema kupitia Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), halmashauri na vijiji wanaendelea kulinda misitu iliyopo kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya mvua, vyanzo vya maji.

Habari Kubwa