Mamlaka zaelekezwa utoaji leseni za uvuvi

20Sep 2019
Renatha Msungu
MULEBA
Nipashe
Mamlaka zaelekezwa utoaji leseni za uvuvi

SERIKALI imezitaka mamlaka zinazohusika na utoaji wa leseni kwa mazao yatokanayo na sekta ya uvuvi kwa wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali za samaki wilayani Muleba mkoani Kagera.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

Pia zimeagizwa utolewaji wa leseni hizo ufuate taratibu bila kuvunja sheria na kukwepa kulipa kodi.

Maelekezo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alipokuwa akizungumza na wavuvi  na wachakataji wa samaki ili kutafuta ufumbuzi wa namna ya kuongeza uzalishaji wa thamani kwa pato la Taifa kupitia sekta ya uvuvi inayoonekana kuwa na kiwango cha chini cha uzalishaji ikilinganishwa na Uganda na Kenya.

Ulenga alisema mamlaka hizo ziache wananchi washindane katika biashara ya kuuza mazao ya samaki ilhali mradi wa leseni ya biashara ifuate taratibu za ulipaji mapato na kuonyesha kuwa taifa linapata mapato ya kukuza uchumi wake.

“Acheni watu wapambane kufanya biashara iwe za mifupa, mabondo, vichwa vya samaki, dagaa ilhali amepatiwa leseni ya biashara ambayo itamtaka alipie mapato ya zao analofanyia biashara,” alisena.

Alisema lengo ni kuona pato la serikali linainuka pamoja na uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.

Alisema mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la Taifa unakadiriwa kuwa asilimia 1.5 hadi tatu kutoka katika Ziwa Victoria kutokana na  samaki aina ya sangara, sato, dagaa na wengine, na kwamba  kwa mwaka mmoja kwa nchi tatu ni Sh. trilioni  sita.

Aidha, Ulega alisema licha ya kuwa Tanzania kuwa na eneo kubwa la Ziwa Victoria kwa asilimia 51 wakati  Uganda ni 43 na Kenya ni asilimia sita pekee, nchi zinavua kwa kiwango cha juu na mapato, lakini Tanzania uzalishaji ni kidogo.

"Wenzetu wana eneo dogo sana, lakini uzalishaji wa thamani kwa makadirio kwa mwaka mmoja pekee ni mkubwa ukiangalia sisi tuna eneo kubwa asilimia 51, lakini bado tuko nyuma," alisema Ulega.

Habari Kubwa