Mlemavu aliyepelekwa shule mgongoni mwa mama amiliki kampuni ujenzi

20Sep 2019
James Lanka
MOSHI
Nipashe
Mlemavu aliyepelekwa shule mgongoni mwa mama amiliki kampuni ujenzi
  • Achukia kupitiliza unyanyapaa kwao
  • Akumbuka mateso alipothubutu ajira

ELIMU, ajira na ujasiriamali kwa wenye ulemavu ni mambo ya msingi ya maisha ambayo yamekuwa yakipuuzwa na wazazi, jamii na serikali kwa ujumla, hivyo kuwaacha katika ‘kiza kinene.’

Mkurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi ya Mchamchaka Construction na mwanzilishi wa asasi ya kusaidia watu wenye ulemavu ya Miembeni Action and Passion for People with Disability, Hussein Msacky, mwenye ulemavu wa viungo akiwa ‘saiti’ na mafundi wake.

Moja ya vikwazo hivyo, ni huduma sahihi za miundombinu kutokana na mahali waliko.

Pia familia zinazoamini ulemavu ama ni laana au mkosi, jambo linaloacha baadhi ya wanafamilia wenye mawazo duni, wanawaficha watoto wao.

Hilo likirejeshwa katika historia ya uvumilivu hadi mafanikio ya kijana mjasiriamali msomi ngazi ya shahada, Hussein Msacky, ambaye ni mlemavu wa miguu, hali ni tofauti, kwani amepiga vita hayo kwa vitendo na kuvuka vikwazo mbalimbali vizito vilivyomsibu katika safari ya hali yake.

AIBUKIA NGO

Mafanikio ya safari yake tangu elimu ya msingi hadi sekonbari, leo hii anamiliki kampuni ya ujenzi, sambamba na kujaribu kuwanyanyua wanaofanana naye, akianzisha asasi isiyo ya kiserikali iitwayo Miembeni Action and Passion for People with Disability.

Anasema, lengo la asasi hiyo ni kuwasaidia wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali za kijamii, kichumi na hata kisiasa.

Msacky, ameiambia Nipashe  katika mazungumzo maalumu mjini hapa, kuwa asasi hiyo inatarajia kutoa elimu endelevu kwa familia zenye watu walemavu mkoani Kilimanjaro, waondokana na unyanyapaa, pia ukiukwaji wa haki zao.

Msacky anasema unyanyasaji kwa wenye ulamavu ni wa asilimia kubwa na huanzia kwenye ngazi ya familia, hivyo kupitia asasi tajwa wameamua kujikita katika utoaji elimu maalumu ya haki zao.

Anasema, walemavu wanapaswa kupewa nafasi mbalimbali katika kizazi kilichopo, kwani ‘wanaweza ikiwa watawezeshwa’ na siyo kufichwa majumbani.

“Uchunguzi uliofanywa na asasi yetu tumegundua kuwa, unyanyasaji mwingi kwa watu wenye ulemavu kama kufichwa kwa kufungiwa ndani ya nyumba, huanzia majumbani mwao,” anafafanua Msacky.

Mkurugenzi huyo anasema, binafsi amepitia changamoto mbalimbali tangu masomoni, shule za msingi hadi chuo kikuu, hata kufikia hatua ya kumiliki kampuni sasa, akiamini ulemavu siyo sababu ya kuwaficha au kuwanyanyapaa.

“Tutaanza kutoa mafunzo hayo kwa familia, baada ya hapo tutahamia kwa watu wenye ulemavu wa namna tofauti na kisha jamii yenyewe kwa ujumla, ili waweze kuzielewa na kuzitambua vyema haki za watu wenye ulemavu,” anafafanua malengo yao.

Anaendelea kwamba, mazingira aliyopitia, anaamini wapo watu wengi wenye ulemavu kama wake ambao wakitunzwa vizuri, wana mchango mkubwa katika jamii zao.

Rai ya Msacky kwa wazazi na walezi ni kwamba, wasiwafiche watoto wenye ulemavu na badala yake wapelekwe shuleni kama walivyo watoto wengine wasio na ulemavu, kwani nao wana haki ya kupata elimu.

Anafafanua kwamba serikali imeweka mpango mzuri wa kuwapa kipaumbele watoto wenye ulemavu, hivyo ni jukumu la mzazi kuhakikisha mtoto mlemavu anapata elimu sawa na wengine.

MAPAMBANO YAKE

Akielezea alivyoweza kupiga hatua, licha ya ulemavu wa viungo, mwanaharakati huyo wa haki za walemavu wenzake, anatembea kwa kutumia kiti cha magurudumu mawili, anasema amepitia historia yenye changamoto lukuki, kutokana na ulemavu wake.

Hiyo ni katika safari ya maisha tangu kuisaka elimu shuleni hadi chuo kikuu, kusaka ujuzi na hatimaye kujiajiri na kuajiri vijana wengine ndani na nje ya Manispaa ya Moshi, kupitia kampuni yake ya ujenzi.

Msacky anaiambia Nipashe kuwa, alikotoka na alikofikia, pia anakoenda ni kwamba, amefungua kampuni akishirikiana na ndugu zake, baada ya kukabiliana na changamoto akitaja mtazamo wa kumbagua kwa sababu ya ulemavu wake ulitawala huko nyuma.

“Kama unavyojua, watu wenye ulemavu tunaonekana kama mzigo katika jamii na hata mimi nakumbuka baada ya kumaliza masomo yangu ya uhasibu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), jijini Dar-es-Salaam mwaka 2011. Nilisota sana pasipo kupata ajira kutokana na hali yangu ya ulemavu,” anasimulia Msacky.

Mwekezaji huyo msomi wa biashara, anakumbuka mwishoni mwa mwaka huo alipata kazi katika kampuni moja jijini Dar-es-Salaam, katika nafasi ya uhasibu, hali iliyomfanya alazimike kumwajiri mtu wa kumsukuma kwenye kiti.

Anasema, hiyo ilikuwa safari kutoka nyumbani hadi kazini na kumpandisha na kumshusha ghorofani, kutokana na miundombinu ambayo haikuwa rafiki kwake katika ofisi zao.

“Kutokana na hali hiyo kulazimika kutumia fedha kidogo nilizokuwa nazipata kumlipa mtu wa kunipeleka na kunirudisha kutoka kazini, niliacha kazi katika kampuni hiyo na kurudi nyumbani Moshi.

“Niliajiriwa kama mhasibu msaidizi katika kampuni moja ya utalii, ambako huko nilikabiliana na changamoto nyingi za kimiundombinu, kutokana na aina ya ulemavu wangu na sikujali hilo, ila changamoto nyingine kubwa iliyonikera sana ni unyanyapaa,” anasema Msacky.

Anaendelea kufafanua kwamba, alipambana huku akielekeza imani yake katika msaada wa Muumba na ndipo alipopata wazo la kujiajiri, kwa kushirikiana na ndugu yake ambaye kitaaluma nia mhandisi ujenzi, wakaanzisha kampuni  iliyopo sasa.

Anarejea masomo yake katika Shule ya Msingi Mawenzi, katika Manispaa ya Moshi mwaka 1995, alipohitimu CBE mwaka 2011, mama yake mzazi alimtia moyo. Hapo anakumbuka namna alivyobebwa mgongoni, alipokuwa katika Shule ya Msingi Mawenzi, mjini Moshi.

Msacky anasema, ni changamoto itokanayo na kukosekana fedha za kumnunulia kiti cha magurudumu matatu, maalum kwa walemavu.

“Kutokana na kukabiliana na changamoto za kimiundombinu tangu nikiwa mdogo, kwa sasa sijali tena changamoto hizo. Kikubwa napambana nacho ni suala la ‘unyanyapaa’ kwa watu wenye ulemavu.

“Sipendi kabisa watu wanaotunyanyapaa, na ndoto yangu tangu nikiwa mdogo ni kuwa kiongozi mkubwa, ili niweze kuwatetea watu wenye ulemavu Tanzania na ulimwenguni kote,” anasema.

Pia anawashukuru wadau wote wanaoshirikiana naye kwa kumpa kazi mbalimbali tangu alipoianzisha mwaka 2017 na jambo linalomsaidia yeye kutoa motisha kwa  wengine wenye ulemavu kwamba wanaweza.

Msacky anafafanua kuwa, anakusudia kuanzisha taasisi ya kuwawezesha wenye ulemavu kupata vifaa vya kutendea kazi.

JICHO LA UONGOZI

Kuhusu fursa ya uongozi, Msacky anatoa wito kwa serikali kuwapa nafasi watu wa aina hiyo kwa ngazi mbalimbali hata bungeni, ili kutoa uwakilishi hai unaowahusu, kwani anaamini wanaweza kama ilivyo kwake.

“Nachukia sana tabia ya baadhi ya watu kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu, kwani ulemavu siyo ugonjwa na mtu yeyote anaweza kupata ulemavu hata ajali. Ni vizuri serikali ikatoa nafasi nyingi zaidi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kuwasemea wenzao matatizo yao,” anasisitiza.

Katika  historia yake, alishawahi kugombea nafasi ya udiwani, lakini  hakufanikiwa mwaka 2015 na anatoa wito kwa walemavu popote walipo,  wajitume kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.​​​​​​​

Habari Kubwa