Robo karne TGNP na Beijing Mama Mongella akiwapa mawili ya kihistoria

20Sep 2019
Yasmine Protace
DAR ES SALAAM
Nipashe
Robo karne TGNP na Beijing Mama Mongella akiwapa mawili ya kihistoria
  • Hatua za ‘kukokotoa’  uongozi nyumbani na ugenini

MWAKA huu ni wa harakati za ukombozi kwa wanawake.

Balozi  Getrude Mongella akizungumza.

Azimio la Mkakati wa Beijing ukitimiza miaka 25. Ni mpango kazi ulioshtua na kuanza kusukuma harakati za ukombozi kwa wanawake.

Hapo pakashuhudiwa kuanzishwa mashirika mengi nchini ya kijamii kutetea haki za kinamama na watoto. Hapo ndipo penye historia ya kuzaliwa kwa asasi ya utetezi wa haki za kijinsia na watoto – TGNP Mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji  wa taasisi hiyo, Lilian Liundi, anafafanua historia kwamba ilianzishwa mwaka 1993 na mpaka sasa imefikisha miaka 25 au robo karne, katika kumpigania mwanamke na mtoto. Umri rasmi unatimizwa rasmi wiki ijayo.

Anasema, walichoamua katika dhihirisho ambalo katika sura pana linamuinua mwanamke kiuchumi, maandalizi yake ikijumuisha kinamama 1500.

"Tamasha hili litazungumzia masuala ya (mkutano) Beijing (China) ambapo watafanya mikakati ya pamoja na kuona walipo sasa na walikotokea," anasema.

OFISA PROGRAMU

Anna Sangai ni Ofisa wa Programu na Harakati za Ujenzi wa Nguvu za Pamoja wa TGNP Mtandao, anasema lengo la maadhimisho ni kuhakikisha sera mwongozo uliopo unafuatwa.

Mama huyo anaeleza TGNP Mtandao ilianzishwa na wanachama wachache waliohudhuria mkutano wa Beijing, wakilenga kuwatetea wanawake na haki zao.

“Mwaka 1991  hadi 1995 watu waliratibu safari kwa ajili ya kwenda Beijing,” anasema Anna, mwenye taaluma ya ualimu na anafafanua zaidi: "TGNP ilianza na sera moja ya kukusanya taarifa na kusambaza taarifa zinazohusu masuala ya jinsia."

Anarejea mzizi wa historia iliyopo, watu wengi hawakujuwa dhana za jinsia na kuona kama neno linalomuhusu mwanamke pekee.

Kutokana na hilo, anasema idara ya pili ilianzishwa baada ya kuonekana uhitaji wa kufahamika kwa kina masuala ya kijinsia, ndipo TGNP Mtandao ikaanza kutoa uelewa kwa makundi mbalimbali, serikali na asasi za kiraia.

Anasema, idara ya tatu ilisaidia ushauri na utetezi, kusukuma mabadiliko ya kutoa ushawishi na utetezi katika sera, baada ya kuonekana mkwamo wake.

"Hamasa imekuwa kubwa na watu wameanza kufahamu na sasa kuna klabu za masuala ya kjinsia katika shule za msingi na sekondari," anasema.

CHANGAMOTOAnataja changamoto yao  kwamba, wanafanya ushawishi wa kisera na bajeti, lakini utekelezaji unakwama, kwani  fedha zinazotengwa kutetea jinsia ni ndogo.

Pia anazungumzia ufuatiliaji duni, wakati wao wanaharakati wahitaji kuwa na kundi kubwa la jamii yenye ufahamu sahihi wa masuala ya jinsia, hali ni kinyume.

Anna  anaenda mbali, akitaja mila na desturi katika jamii nayo ni changamoto , kwani inapunguza idadi ya wanawake wasomi, kwani hawapati fursa za kusoma.

TAMASHA LIKOJE?

Ofisa Habari wa TGNP Mtandao, Monica John, anasema tamasha la jinsia linawakutanisha wanawake wa maeneo mbalimbali na kupaza sauti zao, kuhusiana na maisha ya kinamama.

Anafafanua: "Tamasha ni la 14 kwa mwaka huu kufanyika. Ni kubwa na litakuwa linasherehekea miaka 25 ya TGNP Mtandao, pia kuelimisha jamii kuhusu miaka 25 ya mikakati ya Beijing."

Monica anaeleza malengo yaliyoko ni kutafakari na kupeana taarifa za kujifunza, kuzitambua nyanja mbalimbali na mada kuu ni “Harakati za wanawake zinavyoweza kuleta mabadiliko.”

Anasema, mbali na mijadala, washiriki wataleta bidhaa zao, watabadilisha mawazo kupitia bidhaa hizo, kutokana na kuelekea uchumi wa viwanda.

Deo Mushi, ni mdau mwingine kutoka TGNP Mtandao anayesema maazimio 12 yaliyofikiwa jijini Beijing, wameyafikia katika kusaka haki za wanawake.

Kwa mujibu wa Mushi, eneo mojawapo la kisera ni kuwaelimisha wanawake kiuchumi, katika mtazamo wa kumwengua kutoka katika umaskini.

MAMA MONGELLA

Getrude Mongella, aliyesimamia Mkutano Mkuu wa Wanawake Duniani na mdau mwasisi wa TGNP Mtandao, anadokeza undani uliowafikisha kinamama waliko sasa.

Anasema, kikao cha TGNP Mtandao kinalenga kila atakayejua simulizi ieleweke katika kada tofauti ya vijana, wakiwamo wanafunzi waliopo vyuoni, pia kinababa wengi hawajui vyema historia ya Beijing.

"Sasa leo watapata simulizi juu ya Beijing, tunaamini kuwa ile simulizi inaleta picha na kujua nini kilichosababisha watu kwenda Beijing. Huu ni mwaka wa 25 kuhusu safari ya Beijing," anasema.

Getrude anasema, kinamama wa Kiafrika walipigania haki na usawa katika mapambano yote ya kudai uhuru wa kinamama wa Kiafrika walipambana.

Anasema wamepambana katika kumkomboa mwanamke kwa kuwa walimu wengi ni wanawake, huku akilalamika wamesahaulika kuwekwa katika vitabu vya historia, wakati alichangia kutengeneza historia hiyo.

Kiongozi huyo mstaafu, anasimulia harakati zake za kuwania uongozi, akianza hati ya kugombea uenyekiti wa tawi na akajitosa kugombea nafasi kama hiyo kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ngazi ya mkoa na akafanikiwa.

Mama Getrude hafichi upendo wake kwa asasi hiyo ya TGNP akisema alikwea zaidi kufanikiwa kufikia Rais wa Bunge la Afrika Mashariki katika mapambano aliyokumbana na waliombeza kugombea nafasi hiyo.

Anasema, hakukata tamaa na alifanikiwa kutwaa nafasi hiyo na historia ikaenda mbali, hadi kuwa Mkuu wa Mkutano wa Kimataifa wa Nne wa Umoja wa Mataifa, uliofanyika Beijing, China.

Getrude anasema ni kikoa kilicholeta mapendekezo ya uhusiano wa wanadamu; wanaume na wanawake.

Asen Muro ni Mwenyekiti wa TGNP Mtandao, anayemsifu Getrude, kwamba amewainua wanawake wengi katika mapambano yao nchini mwao, barani Afrika.

Kwa mujibu wa Getrude, mapambano yalitokea kwa sababu uhusiano haukuwa sawa na anafafanua: "(mwaka) 1949 Umoja wa Mataifa ulisema wanawake na wanaume wapo sawa, baada ya tamko hilo mwaka 1975 Umoja wa Mataifa ukatangaza Siku ya Wanawake Duniani."

Anasema, katika mkutano uliofanyika nchini Mexico, wa kwanza ulifanyika mwaka 1975 na uliwaleta wanawake na wanaume kuwa kitu kimoja. Ni mkutano ulioongozwa na wanawake katika kudai haki zao.

Anaongeza kuwa mkutano huo ulitoa tamko la kuwapo maazimio 10  kwa wanawake, ikihusisha usawa kwa wanawake waliotajwa  kuchangia kuleta maendeleo ya nchi.

Kwa mujibu wa Mama Getrude, mkutano wa pili nchini Denmark, walikubaliana kufuta ubaguzi kwa wanawake wa nchi zote, hasa kupitia elimu, nafasi sawa ya ajira na huduma muhimu kama za afya.

Anasema, mkutano wa tatu ulifanyika jijini Nairobi mwaka 1985 anaokumbuka walisumbuliwa katika kudai haki zao, kwa kuwa wengi walikataliwa haki ya kuhudhuria mkutano huo.

Getrude anamsifu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kwamba alisisitiza lazima waende ana anaendelea:"Tuliruhusiwa wanawake wengi kwenda na hapo tulikuja tukiwa na ajenda dhidi ya mapambano." 

Anasifu ni mkutano uliosaidia kuwapo siasa na kuwekwa katika sehemu za maamuzi. Baada ya hapo wakaenda na ajenda ya kumlinda mwanamke na walifanya utafiti, wakagundua wasichana wengi wanabaguliwa na familia zao.

Habari Kubwa