Ajiua kisa kamari imemlia mil. 103/-

20Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ajiua kisa kamari imemlia mil. 103/-
  • Atafuna urithi, mama hana makazi

MWANAMKE kijana raia wa Uingereza, amefariki baada ya kucheza kamari iliyommalizia fedha zote, paundi 36,000 ambayo ni sawa na dola 45,000  au Sh. milioni 103 na laki tano.

Kimberley Wadsworth.

Katika matumizi hayo, paundi 17,000 ilikuwa kutoka urithi wa bibi yake.

Kimberley Wadsworth, mwenye umri wa miaka 32 alimwomba mama yake fedha za kulipa madeni katika mchezo huo, hali iliyomwacha mama yake bila sehemu ya kuishi.

Alianza kucheza kamari katika sehemu za starehe na kwenye mitandao mnamo mwaka 2015, alipopata sonona, baada ya kifo cha baba yake na kuwa na ndoa isiyokuwa na furaha.

Mtoto huyo alijaribu kumficha mama yake mwenye umri wa miaka 65 juu ya hali yake hiyo na ikashindikana.

"Hakulipa deni hata moja, bali aliendelea kucheza kwa muda wa wiki mbili mfululizo hivyo nikabaki bila mahali pa kuishi," anaeleza mama yake ambaye alipotambua tatizo hilo, alijaribu kumtafutia mtaalamu wa afya ya akili amsaidie, lakini hakwenda.

Badala yake alimwandika ujumbe mama, ‘tumechelewa sana mama’ kabla hajajiua.

Nchini humo, kunaelezwa tatizo hilo ni kubwa sana hata kuhatarisha maisha ya wengi kudhamiria kujiua, huku takwimu ikitajwa kuwa wapo wapatao 340,000 wenye tatizo kubwa la uraibu wa kamari.

Hivi sasa kuna vituo kadhaa vya afya vimeanzishwa nchini humo, ili kuwasaidia watu walioathirika na tatizo la kamari.

Inaelezwa ‘ulevi’ wa kamari huongezeka kadri mtu anapozidi kupata fedha nyingi, kwani kuna simulizi nyingine  ya kijana aitwaye Chris Murphy, alianza kupata hali hiyo alipopata paundi 350 akiwa na umri wa miaka 17.

Tangu wakati huo mpaka alipofika miaka 23, alishatumia zaidi ya paundi 100,000 katika kamari, huku afya yake ya akili haikuwa salama.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, jambo la muhimu katika kukabili hayo, ni kumtaka mtu mwenyewe kupambana kuacha mchezo huo wa kamari, anaodhani hawezi kuuacha na hakuna ubaya kwa mtu kukubali kuwa anahitaji msaada.

Inaelezwa, huenda mtu kuacha kucheza kamari ni jambo gumu zaidi ya mtu kuamua kuacha dawa za kulevya au pombe.

Inatahadhariswa, kamari inaweza kumfanya mtu afilisike, kupoteza uhusiano mzuri na wapendwa wake, kupoteza ajira na kupata msongo wa mawazo.

Habari Kubwa