Stendi mpya ilivyobeba kilio cha abiria mjini Nachingwea

20Sep 2019
Sabato Kasika
NACHINGWEA
Nipashe
Stendi mpya ilivyobeba kilio cha abiria mjini Nachingwea
  • DC:Vumilieni, miundombinu kote
  • Mabasi 60, taa kote, vibanda 50 vyaja

KWA aliyefika stendi ya mjini wa Nachingwea mkoani Lindi, kabla ya Agosti 10 mwaka huu, mtu akihoji kulikoni kuhusu uhalisia wa stendi ya mji huo, basi jibu ni dogo sana kwamba ni maarufu, tena hapafikii hata ukubwa wa nusu uwanja wa mpira, kila mahali pamejaa vumbi tupu.

Baadhi ya mabasi yanayoenda safari fupi yakiwa katika stendi mpya.

Mahali hapo ndiko ‘siku nenda rudi’ pamedumu pakibeba umaarufu wa sifa ya stendi kuu ya mji huo mkongwe wenye mambo mengi ya kihistoria, katikati ya mji. Hiyo ni Nachingwea kongwe ambayo ‘kipenga pyeee’ cha kupatikana Uhuru wa Tanganyika, mnamo Desemba 9 mwaka 1961, mahali hapo palishakuwa wilaya.

Leo ikiwa zaidi ya mwezi mmoja, maisha na tafsiri ya  stendi hiyo siyo moja pakoje? Nikiwa miongoni mwa abiria waliozoea kushuka kwenye stendi hiyo, lakini niliangukiwa na butwaa Agosti 30 mwaka huu, hapakuwa hivyo.

Nilipatwa na mshangao baada ya kuwasili mjini Nachingwea nikiwa na mtazamo basi litafikia stendi ya zamani, kumbe siko. Lilipitiliza stendi hiyo kongwe, kuelekea nje ya mji kwenye stendi mpya. Ni hali iliyonifanya nijidadisi ‘kichwani’ kwanini tupitilizwe?

Baada ya mwendo wa umbali fulani, nikaambiwa ndiko kwenye stendi mpya. Huko niliukuta uwanja mkubwa wa vumbi la wastani na kwa jicho la haraka, ukubwa wake ni wastani wa viwanja vitano vya mpira. Ni mahali penye mabasi kadhaa na bodaboda.

Nikasikia malalamiko ma minong’ona kutoka kwa baadhi ya abiria wenzangu kuhusu hatua ya kupitilizwa mjini hadi stendi hiyo mpya, kwamba ‘watarudije huko’ na nilipodadisi kwa kutumia uwanahabari, nilibaini mabasi yameelezwa kushusha abiria eneo hilo kisha yanarudi kulala stendi ya zamani.

Hiyo ndiyo Nachingwea mpya inayoandaliwa katika mpango mji wa Mkuu wa Wilaya, Rukia Muwango, ambaye Nipashe, ilichukua hatua kumhoji kulikoni?

 DC AFAFANUA

"Maendeleo yana changamoto zake, hivyo abiria na Wanachingwea kwa ujumla hawana budi kuvumilia hali hii wakati serikali ikiendelea kuboresha huduma za usafiri," anasema Rukia.

Anakiri kupokea malalamiko ya umbali wa stendi kutoka kwa watu mbalimbali, lakini hawezi kukubali abiria washushwe kwingineko. Anawasihi wakazi wakubaliane na uhalisia kwa ajili ya maendeleo yao, vinginevyo ni kurudisha nyuma juhudi za viongozi wao.

"Tukisema abiria washuke stendi ya zamani au katikati ya mji, maana yake ni kuruhusu watu kutoizoea stendi mpya. Tumeamua wote washuke kule stendi mpya na kisha kila mmoja aende na njia zake," anasema.

Mkuu wa Wilaya huyo anasema, mji wa Nachingwea unazidi kukua na ndio sababu ya kujenga stendi mpya pembeni mwa mji, akiwa na uhakika itazoeleka, pindi itakapokuwa na  huduma zote za msingi.

"Bado ni mapema mno, ndio maana baadhi ya abiria wanalalamika, lakini nina uhakika watazoea tu, kwani maeneo mengi hapa nchini stendi zimejengwa nje ya miji ili kupisha shughuli nyingine za maendeleo," anasema.

Anasema mwanzoni baadhi ya abiria na wasafishaji walikuwa wanatishia kuandamana kususia kutumia stendi mpya kwa sababu ya kutokamilishwa miundombinu, ikiwamo sehemu ya kupumzikia abiria.

“Sasa jengo la kupumzikia abiria lipo na serikali inaendelea kuboresha stendi hiyo kila inavyowezekana, ili kuhakikisha inakamilika yote na nirudie kuwataka abiria kuwa wavumilivu," anasema.

ABIRIA WALALAMA

Kuna malalamiko ya abiria wanapodai kushushwa mbali na wanalazimika kutumia usafiri wa bodaboda kurudi katikati ya mji, hali inayowaongezea gharama zisizo za lazima.

Agosti 30 mwaka huu, Nipashe ilishuhudia namna madereva wa bodaboda wakichangamkia abiria kuwatoza nauli ya Sh. 3,000 na Sh. 5,000 kwa kila abiria.

"Kwanini wamehamisha stendi kutoka mjini, halafu haturuhusiwi kushuka njiani. Tunaletwa huku na kulipa nauli nyingine ya usafiri wa bobaboda," analalamika msafiri anayejitambulisha kwa jina, Somoe Juma.

Pia Shaban Mrope, analalamika sababu ya kutokuwapo mbadala wa mabasi yangefika stendi mpya kisha yarudi na abiria wanaoshukia mjini, kuliko kuwaacha huko.

"Tunashushwa huku, halafu basi linarudi tupu mjini kwenda kulazwa kwenye  stendi ya zamani ambayo hatutakiwi kushuka hapo...tunaongezewa gharama," analalamika.

Katika sura nyingine, madereva wa bodaboda wako kinyume wakifurahia kuwa ‘kipindi cha mavuno’ hasa kutokana na ukweli kwamba anayeshuka stendi hiyo analazimika kutafuta usafiri wa kumrudisha mjini.

Usafiri unaopatikana stendi hiyo ni wa bodaboda na mmoja wa madereva ambaye alimbeba mwandishi, Juma Hamis anasema nauli wanayotoza ni halali kutokana na eneo ilipo stendi hadi mjini.

Madereva hao wanasema hali hiyo kwao ni fursa kwa vile wanaingiza kipato kikubwa kwa kusafirisha abiria kutoka mjini hadi stendi hiyo mpya au kuwatoa stendi mpya kwenda mjini kwa Sh. 3,000 hadi Sh. 5,000.

"Siku za nyuma anaweza kushinda kutwa nzima na kuambulia fedha kidogo, lakini kwa sasa angalau tunaingiza kingi, kwani abiria wanaoshuka hapa stendi ni lazima wachukue usafiri wa bodaboda," anasema Hamis.

MHANDISI AFAFANUA

Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Khalifa Kimbendera, anaeleza stendi husika ilianza kujengwa mwaka 2009 na kutumika mwaka 2013, lakini kutokana na sababu zilizo juu ya uwezo wao, waliifunga.

Anasema, stendi ilifunguliwa upya Agosti 10 mwaka huu, ingawa miundombinu yote bado haijakamilika, lakini ana uhakika baadaye kila kitu kitakuwa sawa, kwa vile kazi ya uboreshaji bado inaendelea.

Mhandisi huyo anataja sababu ya kuhama kutoka mjini, ni kwamba stendi ya zamani ilikuwa ndogo na sasa hakuwa na uwezo wa kuchukua mabasi mengi, hivyo wakaona ni bora ianze kutumika mpya huku maboresho ya sasa yakiendelea.

"Stendi mpya ina uwezo wa kuchukua mabasi zaidi ya 60 itakapokamilika na itakuwa imezungukwa na vibanda vya biashara na huduma zote za muhimu kuanzia chakula, nyumba za wageni," anasema Mhandisi Kimbendera.

Anataja huduma nyingine kuwa ni za fedha, choo na anafafanua kuwa halmashauri itajenga vibanda 50 vya biashara vitakavyokodishwa, ili fedha kwamba zitakazopatikana ziweze kuhudumia stendi hiyo.

"Halmashauri tutajenga idadi hiyo ya vibanda na 26 vitakamilika, hivi karibuni na pia tutagawa maeneo kwa wafanyabiashara ili nao wajenge vya kwao na tumeshapokea maombi ya watu 60," anasema.

Mhandisi Kimbendera anasema, stendi hiyo itakapokamilika itakuwa ya kisasa na mfano kwa mikoa ya Kusini, akiwataka abiria na wengine kukubaliana na hali ilivyo kwa sasa.

Anasema, mipango yao inalenga kukamilishwa ndani ya miaka mitatu, pia kutegemea mapato ya halmashauri kama imefanikiwa kukusanya fedha za kutosha kupitia vyanzo vyake vya mapato.

"Stendi itafungwa taa za usalama kila kona na kutakuwa na huduma ya maji na nyingine zote za msingi na itachangamka tu, ingawa kwa sasa baadhi ya watu wanaiona kama haifai," anasema.

Habari Kubwa