Wadau wamlilia Jeba, azikwa Z'bar

20Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Wadau wamlilia Jeba, azikwa Z'bar

RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu, pamoja na wadau mbalimbali nchini wamesikitishwa na kifo cha kiungo wa Chuoni, inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar, marehemu, Ibrahim Rajab "Jeba".

Rais wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Seif Kombo Pandu.

Kiungo huyo wa zamani wa Simba, Azam FC na Mtibwa Sugar za Tanzania Bara, Jeba, alifariki juzi na jana mchana alizikwa katika makaburi yaliyoko kwenye kijiji cha Ndijani, Mkoa wa Kusini Wilaya ya Kati Unguja.

Marehemu Jeba alifariki akiwa kwenye hospitali ya Mnazi Mooja alikokuwa akipata matibabu kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Akizungumza na gazeti hili, Pandu, alisema kuwa ZFF inasikitika kupoteza mchezaji huyo ambaye alikuwa na kipaji kizuri na mchango wake bado ulikuwa unahitajika.

"ZFF tunapenda kutuma salamu za rambirambi kwa familia na ungozi wa timu ya Chuoni, kufuatia kifo cha mchezaji wake, Ibrahimu Jeba kilichotokea hapo jana (juzi)," alisema Pandu.

Taarifa iliyotolewa na Azam FC, ilisema kuwa klabu hiyo imepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji huyo na inaungana na Watanzania wengine katika kuomboleza msiba huo.

Habari Kubwa