PM aagiza majeshi EAPCCO kuimarisha ulinzi mipakani

20Sep 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
PM aagiza majeshi EAPCCO kuimarisha ulinzi mipakani

WAZIRI Mkuu, Kasim Majaliwa, ameliagiza Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi 14 za Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), kuimarisha ulinzi kwenye mipaka ili kudhibiti wahalifu wanaokwepa ukaguzi.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa.

Aliwaagiza wakuu hao kuongeza juhudi kwa kuwajengea uwezo watendaji wao kitaaluma na hoja kwenye serikali zao ili kupata vifaa na vitendea kazi vya kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyokwenda sambamba  na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) duniani.

Alitoa maagizo hayo jana jijjini Arusha wakati akifungua mkutano wa 21 wa EAPCCO kutoka nchi hizo kwa niaba ya Rais John Magufuli.

"Wahalifu wengi wamekuwa wakikwepa ukaguzi kwenye mipaka rasmi niwahimize mwendelee kidhibiti mipaka ya nchi zetu kwa kufanya operesheni za pamoja mara kwa mara, kubadilishana taarifa za uhalifu na wahalifu, kufanya mafunzo ya pamoja na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji kwa kufanya upelelezi kwa pamoja," alisema.

Aliagiza nchi hizo kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji bila kujali mipaka ya nchi wanachama kwa kuwa wahalifu wanatumia udhaifu wa kukosekana kwa ushirikiano madhubuti wa nchi hizo.

"Kuondolewa kwa vikwazo vingi visivyo vya kiforodha, kumesababisha athari za kiusalama na wahalifu wanatumia fursa hiyo kuimarisha magenge yao ya uhalifu unaovuka mipaka, ikiwamo dawa za kulevya, ugaidi, utengenezaji na utoaji wa bidhaa bandia, uharamia katika maziwa na bahari, wizi wa magari, ujangili, utoroshaji wa madini na biashara haramu ya binadamu yanayoambatana na utakasaji wa fedha zinazotokana na uhalifu huo," alisema.

Majaliwa alisema vitendo vya uhalifu visipodhibitiwa ipasavyo vinaleta athari kwa maendeleo na ustawi wa nchi wanachama, hivyo ni vyema wakaweka mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge yote ya uhalifu unaovuka mipaka ili wasipate mahali salama pa kufanyia uhalifu huo.

Kuhusu teknolojia alisema moja ya changamoto kubwa  zinazoukabili ukanda wa nchi hizo, ni kukua kwa teknolojia ya Tehama na mapinduzi hayo yanaleta mbinu na aina mpya ya uhalifu, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa wataalamu waliobobea katika teknolojia hiyo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na utashi wa kisiasa na ili kuondokana na changamoto hiyo utashi wa kisiasa unahitajika ili kuvipa nguvu vyombo vya dola katika kusimamia sheria.

"Niwatake wanasiasa wengine tutoe ushirikiano kwa vyombo hivi ili viwe na meno kwa kutunga sheria zitakazowawezesha kufanya kazi zao ipasavyo," alisisitiza Majaliwa.

Changamoto nyingine alisema utofauti wa sheria baina ya nchi wanachama unatoa mwanya kwa wahalifu kufanya uhalifu kwenye nchi moja na kukimbilia nchi nyingine ambayo haiwabani.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni udhaifu wa utunzaji kumbukumbu za wahalifu katika kanzi data za Interpol pamoja na vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watendaji hali inayosababisha ugumu wa upelelezi na ukamataji wahalifu.

Pia alimpongeza Mwenyekiti mpya wa EAPCCO ambaye ni Mkuu wa Jeshi nchini (IGP) Simon Sirro na kumwagiza kusimamia utekelezaji wa mipango na mikakati ya maadhimio ya mkutano huo wa 21.

Awali IGP Sirro akimkaribisha Waziri Majaliwa, alisema mkutano huo ulitanguliwa na kamati ya utendaji mbalimbali ambazo maazimio na mapendekezo yao yatapitishwa leo na Mawaziri wa Mambo ya Ndani toka nchi hizo wanachama.

"Nawashukuru wakuu wenzangu wa nchi wanachama kwa kuniamini na kunipa uenyekiti kwa kipindi cha mwaka mmoja na nitasimamia amani na usalama katika nchi zetu," alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Interpol, Jurgen Stock, alisema ofisi yake itaendelea kufadhili mafunzo mbalimbali kwenye shirikisho hilo ili ziweze kudhibiti vitendo vyote vya uhalifu.

Mwenyekiti wa EAPCCO aliyemaliza muda wake, Luteni Generali Adil Mohammed, alishukuru wakuu wenzake wa polisi kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake cha uongozi na kuomba wautoe kwa mwenzake.

Habari Kubwa