Zahera aisuka tofauti Yanga

20Sep 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zahera aisuka tofauti Yanga
  • ***Lengo ni kuhakikisha wanaimarika na kuimaliza Zesco nyumbani kwao...

TUTAWASHANGAZA! KOCHA wa Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesema kuwa anaamini kikosi chake kitapata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia, kutokana na "dozi kali" ya mazoezi wanayoipata wachezaji wake.

KOCHA wa Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera.

Akizungumza na gazeti hili jana, Zahera, alisema kuwa kila siku wachezaji wake wamekuwa wakiimarika na hiyo inatokana na programu za mazoezi wanazofanya.

Zahera alisema kuwa pia amewaandaa wachezaji wake kuongeza umakini katika mchezo huo, ambao timu itakayopata bado mapema, itakuwa imejiweka kwenye mazingira ya mazuri ya kusonga mbele.

Kocha huyo alisema kuwa kikosi chake sasa kimeimarika zaidi, tofauti na walivyokuwa katika mechi ya awali, baada ya baadhi ya nyota wake waliokosekana kurejea kikosini.

"Kuna mambo mbalimbali tunayafanyia kazi, tunajiandaa kuwa na kikosi bora na imara zaidi ya tulivyocheza mechi ya kwanza, tumejua nguvu yao na tumejua tulipokosea, kikubwa kwa upande wetu, tulishajiandaa kwenda kutafuta goli ugenini, hii ilishakaa kwenye mipango yetu, tukifanikisha, tutakuwa tumefanikiwa," alisema Zahera.

Aliongeza kuwa anafurahi kuona kila mchezaji ana morali ya hali ya juu kuelekea mchezo huo wa marudiano na maandalizi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara watakazokuja kucheza mara baada ya kurejea nchini.

"Timu yetu inabadilika, ninamaanisha wachezaji wanaimarika, kuna tofauti kubwa inaonekana kila siku tunapofanya mazoezi, matumaini yetu ni kuwapa furaha mashabiki wa Yanga na Watanzania wapenda mpira," aliongeza kocha huyo.

Kikosi cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini kuelekea Ndola, Zambia Jumatatu, lakini kikitanguliza ujumbe kwa ajili ya kukipokea kikosi chao.

Timu hizo zitashuka kwenye Uwanja wa Levy Mwanawasa Septemba 28 mwaka huu, zikiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 waliyoipata Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Wakati huo huo, wawakilishi wengine wa Tanzania waliobakia katika mashindano ya kimataifa ni Azam FC, ambao nao wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuwafuata Wazimbabwe Triangle United, huku wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Septemba 15 mwaka huu hapa jijini.

Habari Kubwa