Samatta afunguka alivyoitamani Ulaya

20Sep 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Samatta afunguka alivyoitamani Ulaya

MSHAMBULIAJI wa KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji na nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta, amesema kuwa ndoto zake za kucheza soka Ulaya zilichelewa kutimia.

Mshambuliaji wa KRC Genk na nahodha wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Samatta.

Samatta, mshambuliaji wa zamani wa African Lyon na Simba zote za jijini Dar es Salaam, aliliambia gazeti hili kuwa alitamani kuanza kucheza soka la kulipwa mapema zaidi, lakini pia anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hiyo.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, alisema kuwa juhudi zake na hali ya kutokata tamaa, ni moja ya sababu zilizomsaidia kufikia mafanikio.

"Nilitamani kupata nafasi ya kucheza soka Ulaya nikiwa hata kabla ya kutimiza miaka 18, hata hivyo haturuhusiwi kukosoa mipango ya Mungu," alisema Samatta, mshambuliaji wa zamani wa mabingwa wa Afrika, TP Mazembe, ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Samatta ambaye Septemba 4 mwaka huu aliiongoza Stars kutinga hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa Qatar mwaka 2022 kwa kuitoa Burundi, mapema wiki hii alifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza mashindano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mchezo huo, Samatta, aliweka rekodi nyingine ya kufunga bao, licha ya timu yake kupata kichapo cha mabao 6-2 kutoka kwa Red Bull Salzburg ya Austria.

Ili kuhakikisha idadi ya wachezaji wa hapa nchini wanapata fursa ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya, mapema wiki, Samatta alionekana katika picha za video, akimwongoza straika chipukizi, Kelvin John, kujifua wakati alipokuwa Ubelgiji kwa ajili ya kufanya majaribio na KRC Genk, ambayo ilimtumia mwaliko wa kwenda huko.

Habari Kubwa